RIWAYA: Daima
NA: Frank Masai
MAWASILIANO: 0717 738973
SEHEMU YA 2
ILIPOISHIA.
Wakati Fatma anaendelea kuzagaa pale uwani akiitazama nyumba
ile juu ya bati na anga zima la pale alipohamia, alijikuta akigongana na mtu
ambaye hakumjua hapo kabla.
Alikuwa ni mtoto
usawa wake, lakini yeye ni wa kiume na alikuwa kabeba baadhi ya vitu
vidogovidogo vya kupeleka ndani ya nyumba ile.
Akamtazama yule mvulana kwa macho yake machanga, na mvulana
yule akamtazama pia. Macho yao yakagongana. Wote kwa pamoja wakabaki hawana la
kusema.
“Sam peleka vitu ndani,” Ni sauti ya mtoto mwingine ilimsihi
mtoto mwenzake apeleke vitu ambavyo kavikamata mikononi mwake.
Alikuwa Samson, kijana anayelelewa katika mazingira magumu
akiwa na mama yake. Samson akatabasamu mbele ya Fatma, na Fatma akajibu
tabasamu lile kwa kukenua hadi mapengo yake ya mbele yakaonekana. Samson
akaingiza vitu vile ndani.
ENJOY.
Macho ya Fatma, hayakuacha kumfatilia Samson ambaye baada ya
kuingia ndani, naye binti aliingia ndani huku kichwani mwake akili za kitoto
zikiwa zimeenea kana kwamba alikuwa anataka kujua zaidi kuhusu mtoto mwenzake.
Akaingia ndani na kumkuta Sam akiwa anaweka kwa uangalifu
vitu ambavyo alikuwa ameagizwa avipeleke ndani.
“Unaitwa nani?” Fatma alimuuliza Sam na mtoto yule aligeuka
nyuma kwa kasi na kukutana na cheko ya kitoto toka kwa Fatma. “Nimekushtua
eeh.” Alitania na Sam akawa hana budi naye kutabasamu.
“Naitwa Samson,” Akajibu Sam kwa sauti ya kitoto.
“Samson au Sam?” Akauliza mtoto yule mwenye asili ya Kiarabu
na weusi wa Kiafrika.
“Sam wanalikatisha tu! Ila naitwa Samson.”
“Haya Samson. Mi’ naitwa Fatma.” Akajitambulisha mtoto wa
kike.
“Ahaaa! Fatma. Unafanana na mama.” Akaongea Sam huku bado
naye uso wake umepambwa na tabasamu.
“Ndio. Na ndio maana anani…” Mara walikatishwa maongezi yao.
“Wewe Sam, kachukue vitu vingine nje. Unamjua huyo,
utanyongwa.” Mtoto mwenzake aliongea na kumfanya Samson atoke haraka mle ndani
na kuendelea na kazi ambayo ameitiwa huku Fatma kila mara akiwa anamuangalia na
kutabasamu kana kwamba alikuwa anamfahamu Samson kwa muda mrefu..
****
“Baba, yule pale nataka awe rafiki yangu.” Baada ya kazi
kumalizika, Fatma alimfuata baba yake na kumwambia maneno hayo.
Kwa muda huo Sam na watoto wenzake walikuwa wanafuraha baada
ya kupewa ujira wao ambao japo haukuwa mkubwa, lakini kwao waliona kama neema
imewadondokea.
“Hapana mwanangu. Kuna marafiki utawapata, lakini si hawa wa
huku. Kwanza wachafu. Embu angalia, wewe unaweza kucheza na mtoto kama yule?”
Baba yake Fatma, Bwana Abdul, aliongea kwa dharau na kumfadhahisha mwanaye.
“Baba mimi sitaki bwana, nataka yule.” Fatma akadeka na
kumkasirisha baba yake.
“….Embu niondokee hapa.” Abdul alimfukuza mwanaye baada ya
maneno makali aliyompatia kuhusu Sam. Mtoto yule hakuwa na pa kukimbilia zaidi
ya kwa mama yake ambaye naye alikuwa roho juu baada ya kumuona mtoto wake wa
pekee akifokewa kana kwamba alikuwa kafanya kosa kubwa.
“Nyamaza. Usilie mwanangu eeh! Nyamaza, nitamchapa baba
yako.” Alimbembeleza mwanaye, Johari Bin Said Mustapha. Kisha akamgeukia
mumewe, “Usipende kumkera mtoto, nakuomba Abdul.” Johari alijikuta akibwatuka
kwa ukali bila hata kuzirekebisha hisia zake za maumivu. Abdul akajikuta mwenye
kugwaya hasa alipogundua kuwa Fatma ndio jicho na pia moyo wa mkewe. Ni kheri
umchukue yeye Johari, ukamchuna ngozi, ukampaka ndimu na pilipili na kisha
ukambanika, halafu baadaye ukawatupia mbwa wafanye kitoweo kuliko kumsinya
kidogo Fatma hata kama amekosea.
“Johari mke wangu, unamdekeza huyu mtoto, baadae itakuja
kutu-cost.” Aliongea kwa upole Abdul, mume wa Johari.
“Simdekezi. Namlea kwa upendo. Tumuache mtoto naye
ajichanganye na watoto wenzake anaowachagua. This is just a world, you will
never know who is going to burry you.” Johari aliongea kwa hisia akimuelekeza
mumewe kuwa hii ni dunia tu, huwezi kujua ni nani atakayekuja kukuzika.
Ipo hivi, Bwana Abdul ni mtu ambaye haamini kama masikini
wanaweza kumsaidia yeye katika maisha yake. Na imani hiyo ilikuwa inapingwa
vikali sana na mkewe Johari. Hiyo ndio sababu mara nyingi sana watu hawa hukwazana
hasa linapokuja suala la ushirikiano baina ya masikini na matajiri.
“Siku moja utaniamini nachokwambia.”Aliongea Abdul na
kuingia ndani akimuacha mkewe anamuangalia kwa macho yaliyojaa ugwadu wa hasira
pamoja na kisununu.
“Twende ndani mwanangu.” Huo ndio uamuzi aliouchukua yule
mwanadada ambaye alionekana hapendi sana matendo ya mumewe, hasa ya kibaguzi.
****
“Mamaa… Mamaa… Mamaa…” Samson, alikuwa anamuita mama yake
huku kasi ya miguu yake ikiwa kubwa kukimbia kule ambapo nyumba anayoishi na
mzazi wake ipo.
“Nini tena mwanangu?” Aliuliza Mama Samson kwa kihoro
akidhani labda mwanaye anafukuzwa na mtu au labda kuna janga limemkuta.
“Nimekuletea hela mama.” Aliongea Samson baada ya kufika
mbele ya mama yake. Mama wa Samson, akafuta machozi ambayo yalikuwa
yanamuandama kwa sababu ya kupikia kuni ndani ya chumba kidogo mithili ya choo.
Alikuwa kavaa mavazi ambayo hayana hadhi kubwa lakini aliamini kuwa yeye si
kama hao wanaojiita wenye hadhi.
“Nani kakupa mwanangu?” Aliulizwa Samson na mama yake.
“Pale kwenye lile jumba kubwa wanahamia. Tumewasaidia nd’o
wakanipa hiyo.” Aliongea Samson kwa furaha huku akizidi kuusogeza mkono wake
ili mama yake aichukue ile fedha.
Mama Samson akatabasamu kwa furaha na badala ya kupokea ile
hela, alipapasa kichwa cha mwanaye huku akijaribu kutafakari la kumwambia.
“Hiyo ni yako Sam. Kaitumie unavyotaka. Jukumu lako ni
kujitafutia kwa sasa. Lakini jukumu langu mimi ni kukutafutia. Ipo siku na wewe
utakuwa na jukumu hilo, kwa sasa bado hujafikia umri huo. Kwa hiyo
utakachokipata, jua kuwa umejitafutia na sina haki ya kukitumia.” Aliongea mama
yake ambaye alikuwa ni mwema na mwenye sauti ya hekima na utii hata kwa watoto
wadogo.
“Lakini mama, wewe unahitaji hela hii kuliko mimi
ninavyoihitaji. Sina mamlaka na hii fedha kama ulivyokuwa nayo wewe. Kwa nini
usiichukue uifanyie kazi ambayo itatusaidia sote hapa nyumbani?” Wanasema mtoto
wa nyoka ni nyoka. Ni wazi hata Samson alikuwa na ulimi sawa na ule wa mama
yake.
“Unajua nini mwanangu?” Mama Samson, alichutama na kukishika
kichwa cha mwanaye kwa mikono miwili. “Kuna muda unatakiwa kuitambua thamani ya
mzazi. Na kuna muda unatakiwa kujua unathaminiwa na mzazi. Kwa sasa unatakiwa
kutambua kuwa unathaminiwa na si wewe kuthamini japo ni vema unithamini, lakini
si kwa njia hii,” Aliongea bado kwa utulivu yule mama. “Umewasaidia wazazi
wengine, na wao kwa hekima zao, wamekulipa. Lakini haimaanishi kuwa wamekupa
ili uje utumie na mimi bali ukajifariji wewe kwa kazi uliyoifanya.”
“Ndio. Lakini mimi nimekupa wewe kwa sababu sina matumizi
nayo. Nitaenda kuchezea tu huko kwa kula pipi na jojo, lakini wewe unaweza
kununulia mkaa na ukapika kwa uhuru kuliko sasa hivi.” Mama Samson akatabasamu
na kutikisa kichwa kwa maneno ya mwanaye. Akashindwa la kuongea na badala yake
akasimama na kumuangalia tena mwanaye, safari hii kwa upendo zaidi.
“Haya.Nipe, maana umenishinda kwa kutoa hamasa.” Sam
akafurahi baada ya ushawishi kwa kupenya kwenye ukuta mzito wa akili ya mama
yake. Akampa kiasi cha shilingi elfu mbili mama yake na kisha akamkumbatia
kabla hajamuachia na kurudi kwa wenzake kuendelea kucheza. Mama wa mtoto akawa
anamuangalia asiamini kama kapata utatijiri wa njia nyingine kabisa, utajiri wa
mtoto mwenye hekima.
****
Miaka miwili ikaingia. Hali ya umasikini ikawa bado
imetawala kwa Edna, mzazi wa Sam. Aliishi kwa kubangaiza na kiasi alichokipata,
alikuwa anakiweka kwa ajili ya mwanaye kwenda shule. Na hatimaye, Sam akaanza
shule ya msingi akiwa na miaka tisa.
Wakati yeye anaanza shule katika umri ule, tayari Fatma alikwishaanza
shule punde tu alipohamia katika ule mtaa. Urafiki wa hawa watoto ulikuwepo
lakini ulikuwa unapingwa vikali sana na baba mtu. Mara kadhaa Mama Samson, Bi
Edna, alipelekewa onyo na yule bwana kana kwamba mama alikuwa anahusika na
urafiki wa watoto. Mama Sam alikuwa mwenye ulimi wa staha, na wenye
kumuelewesha kila aliyekuwa na sikio. Lakini Bwana Abdul, alikuwa haoni wala
sikio lake halikufunguka licha ya kutiwa ufunguo wa kufunguliwa.
“Mama samahani, samahani sana mama yangu.” Ni sauti ya Johari
kila tukio likitokea ndio ilikuwa inaomba msamaha. Mama wa watu alikuwa mwenye
kutabasamu na kuacha mambo yale yapite. Johari alikuwa anajaribu kumpa pesa
yule mama lakini kwa bahati mbaya, hakuna hela ambayo Mama Samson aliweza
kuikubali. Aliamini msamaha wa kweli unatoka moyoni na si kwa kutumia pochi
zinazokaa kwapani au kwa wanaume kukaa nyuma ya kalio.
“Pesa si kitu mwanangu. Kaa na mumeo, mwambie dunia
inalizunguka jua na pia inajizungusha yenyewe bila kuchoka. Hapa na maana
kwamba, ipo siku atajua thamani ya mtu ni bora kuliko vitu. Sitachoka kuisubiri
siku hiyo, mimi ni dunia.” Maneno hayo yalikuwa yanajirudia mara kwa mara
kichwani mwa Johari. Alishindwa kumwambia mumewe kwa sababu alijua hatotilia
maanani lolote lile.
Watoto wawili wakiwa katika furaha juu ya urafiki wao, huku
upande mmoja wa wazazi ukiwa hautaki hata kusikia habari hizo, wanaamua kufanya
jambo. Jambo ambalo liliweza kuwaweka pamoja kwa muda mrefu sana.
“Sam.” Siku moja binti mwenye umri wa miaka saba, Fatma.
Alimuita rafiki yake kwa kificho getini kwao. Sam akimbilia pale getini na
kumsikiliza. “Unajua baba hapendi urafiki wetu. Sasa tunafanyaje?” Binti
akataka suluhu ya urafiki wao.
“Sijui la kufanya Fatma. Ila nachojua, MUNGU ni mwema kwetu
sote. Hajatuumba ili tusijuane, bali katuumba ili tujuane na ndio maana tupo
hapa leo. Licha ya mimi kukujua wewe na wewe kunijua mimi, pia kanijulisha mimi
Wazazi wako wapo vipi na kakujulisha wewe na wazazi wako juu ya mzazi wangu. Nachoamini
kwa sasa, urafiki wetu utakuwa ni wetu. Hakuna ambaye anatakiwa kuja kati
yetu.” Samson aliongea maneno ya kujiamini bila kujua athali za maneno yake.
“Nimefuahi kusikia hayo Sam. Rafiki ndiye kiongozi sahihi wa
kichwa cha yeyote kwa sababu rafiki ndiye anakuja kukufuta chozi pale familia
yako inapokutoka. Na rafiki ndiye awezaye kukuliwaza pale unapokwazana na
wazazi wako. Hamna mtu wa muhimu kama rafiki. Kama huna rafiki, basi dunia hii
utaiona inaegemea upande mmoja hasa pale unapokwama mahali.” Aliongeza maneno
hayo Fatma na kumfanya Sam atabasamu. “Niahidi utakuwa rafiki yangu DAIMA.”
Akaongeza Fatma huku anatoa kidole chake kidogo kwenye tobo la geti. Samson
akakipokea kidole kile kwa kuunga na kidole chake.
“Nakuahidi utakuwa rafiki yangu DAIMA.” Akajiapisha rasmi
Samson.
“DAIMA.” Akaongea maneno hayo Fatma kama msisitizo.
“Ni DAIMA.” Naye Sam akasisitiza.
ITAENDELEA.
Iko vizur mwendelezo wake vp
JibuFuta