Jumapili, 29 Mei 2016

Riwaya Ya Kusisimua



RIWAYA:  Amka Mama.
MTUNZI:Frank Masai
MAWASILIANO: 0717 738973

“Kwako mama.”Sauti ya kike ilianza kwa kutoa salamu .

“Sauti yako bado imetawala kichwa changu licha ya kutoisikia kwa muda mrefu. Nakumbuka mengi uliyoniambia kuhusu maisha haya.
Maisha yaliyojaa chuki,manyanyaso,wivu usio na kifani pamoja na dharau hata kwa wale ambao umewazidi. Kwa sababu wanacho,wanaona huwezi kuwaambia chochote. Nayakumbuka mengi sana mama yangu”.  Sauti chovu na ya kukata tamaa ikichanganyika na simanzi iliendelea kujieleza mbele ya mwili ambao iliamini kuwa unasikia akisemacho. Aliendelea

“Sidhani kama wajua ni kiasi gani nateseka kwa sasa,ila nafahamu u mwenye kujua uchungu wa mwana na waumia sana kwa jinsi mimi niumiavyo.
Japo hunioni ila naamini wanisikia,na ninajua unaufahamu wa kuyatambua haya maumivu yanayonikabiri kwa sababu yako.

Nayatoa  haya kinywani mwangu huku nikikukumbusha yale uliyowahi kuniambia siku nyingi za nyuma wakati nipo karibu nawe,na wakati ulikuwa unaongea. Ulisema  haya huku akianza kwa kuniita mwanangu na mkono wako wa kuume ukikipapasa kichwa changu,”Mwanadada yule alianza kurudia maneno ya mama yake aliyoambiwa kipindi cha nyuma.

“Bado hujayajua maisha yanaenda vipi japo wajua haya tunayoishi ndiyo maisha. Maumivu niyapatayo kwa ajili yako,kamwe huwezi kuyajua hadi wewe utakapopata mtoto wako.
Wewe ni sehemu ya tumbo langu,kaa ukitambua hilo. Kitovu chako,ni utumbo wangu. Nilichokula mimi na wewe ulikila kwa kupitia utumbo wangu.”

Uliyasema haya mama na hukuishia hapa tu!Uliendelea.

“Wakati nimekubeba tumboni,kama mimi niliumwa,basi nilihofia sana kuhusu wewe kuliko kuumwa kwangu.
Niliyajua maumivu unayoyapata ni zaidi ya mara zote ya ninayoyapata mimi. Nilijitahidi kujihudumia ili nikutoe katika maumivu niliyokubebesha,mwanangu.”Kijana yule wa kike alimaliza kunukuu maneno ya mama yake kipenzi,kisha akaendelea.

“Sikujua uliyasema haya kwa nini mama,lakini najua uliyasema katika kufikisha hisia zako kwangu,hisia ambazo kila mzazi wa kike anapaswa kuwa nazo kwa mwanaye.
Sasa nimekuwa mkubwa wa kuyachanganua mambo ambayo ulikuwa ukiniambia. Lakini licha ya ukubwa nilionao,najua bado nikiumia hapa nilipo na niendako,wewe unaumia zaidi yangu. Wewe ni zaidi ya kila kitu katika maisha yangu.Naomba utambue hili.

Sitaki kujiuliza ni mara ngapi umepigana kwa ajili yangu kwani hata nikijua,siwezi kulipa wala kugusa pale ulipopita wewe. Ni kazi kubwa umeifanya mama yangu,na hii ni kwako mama. Inuka na futa chozi langu kama ulivyolifuta kipindi kile nilipokuwa nalitoa kwa sababu ya maumivu.

Hekima na busara zako ndizo zilizojaza ujasiri moyoni mwangu hata kwa yule ambaye niliwahi kusema sitamsamehe katika maisha yangu. Nataka kukwambia kuwa,nimemsamehe baba na huko alipo,MUNGU amlaze mahala pema peponi.
Japo najua alikuwa akikutenda sana,lakini ulisimamia kidete haki zako. Hata pale alipokupiga usiku wa manane na kukutaka uondoke nyumbani kwake,bado ulinikumbuka na kunikumbatia ili uondoke nami.
Naikumbuka sana ile siku.Nilikuwa nina miaka sita. Ni zamani sana,kwani leo ninamiaka ishirini na nane,miaka ishirini na mbili imepita tangu tukio lile litukie.

Siku ile ilikuwa ni Jumapili kwa kuwa tulienda kanisani mimi na wewe. Sikumbuki ilikuwa ni tarehe ngapi,lakini ilikuwa ni mwezi wa kumi na mbili.
Tulipotoka kanisani na kurudi nyumbani,hatukumkuta baba. Naikumbuka ile siku,nakwambia tena hilo.”Binti aliendelea kukumbusha anayokumbuka.

“Baba alirudi sijui saa ngapi,ila kilichonishtua usiku ule ni kusikia sauti yako ikilia huku mwili wako ukitoa sauti kama ya mtu anayekung’uta vumbi nguo zake.
Nilishuka kitandani ili nije kuona ni nini kinachoendelea usiku ule wa saa tisa na dakika kadhaa. Wakati huo hali ya hewa nje ilishabadilika sana.Wingu jeusi lilitanda,na manyunyu ya mvua taratibu yalianza kusikika kwenye paa la nyumba yetu.

Baada ya kutoka chumbani mlipokuwa mnanilaza,nilikuja hadi pale sebuleni na nilishuhudia kwa macho yangu baba akikuburuta sakafuni huku akikushindilia mateke katika mwili wako kana kwamba anamfanyia hivyo mnyama,au kitu chochote ambacho hakina uhai.
Hakika mama ile picha haijafutika katika kichwa changu. Yale mateke na ngumi alizokuwa anazishusha katika mwili wako,hadi sasa hivi picha ile inatawala ubongo wangu.
Hakika mama nakwambia, sijasahau hata chembe japo hukuwahi kuliongelea suala hili.”Dada yule mrembo aliongea haya na safari hii machozi yalianza kutiririka toka machoni mwake lakini hakuacha kuongea japo sauti iliambatana na hali ya kilio.

“Mama, nashindwa kufahamu nimeumbwaje,ila namshukuru MUNGU kaniumba jasiri kama wewe.
Nilipokiona kitendo kile,nilichomoka kwa kasi na kwenda kushikilia miguu ya baba aache kufanya alichokuwa anakifanya. Lakini kwa akili ambayo alikuwa nayo usiku ule,baba alinisukuma kama mpira wa miguu na mimi nilidondokea pembeni huku nikimuacha akiendelea kukuburuta pale sakafuni.
Sikutaka kukubali kuendelea kukuona unazidi kufanyiwa matendo yale ya kikatiri na mtu ambaye ulimthamini hadi ukamkabidhi maisha yako ayaendeshe.

Nilisimama tena na kwenda kumkamata miguu baba na safari hii niliongezea kumng’ata ili aache kukufanyie yale.
Maumivu yaliyotokana na meno yangu kuingia katika ngozi yake,baba alijikuta akinipiga teke la nguvu tumboni na kunifanya nitoe mlio wa uchungu. Uchungu ambao hakuna ambaye angeuhisi zaidi yako wewe mama.
Na uchungu wangu huo ndio ulikupa ujasiri wa kuinuka pale chini na kumkunja baba kama mtoto mdogo. Baba alipojaribu kujitutumua ulizidi kumfundisha heshima iliyomtoka baada ya kubwia pombe zake. Heshima ambayo kama  angekuwa nayo,asingethubutu kunipiga teke lile wala kukuthurubu wewe.
Hakika nakwambia mama.Wewe ni zaidi ya Komando,wewe ni zaidi ya wale wanaoweza kupindua nchi. Wewe ni zaidi ya kila kitu katika hii dunia. Naomba upokee hizi thamani nazozitoa mdomoni kwangu.
Amka mama,pigana hadi mwisho.Pigania pumzi yako.Nakuhitaji mama,nakuomba amka. Amka na kuniangalia mwanao,niangalie navyotaabika bila ushauri wako. Niangalie tena,amka mama,tafadhali.”Binti yule aliongea hayo kwa uchungu huku akimtikisa mama yake aliyekuwa kalala kitandani katika wodi ya wagonjwa mahututi.
Mipira ilikupita puani na mdomoni huku akiwa hajielewi hata kidogo. Alikuwa ni wa kulishwa na mipira, kupumua kwa mipira na wa kujisaidia hapohapo.
Sasa mtoto wake anajaribu kuongea maneno makali ili kama mama yake yule kipenzi anasikia, aweze kuamka. Lakini kitendo kile cha kumtikisa mama yake kwa nguvu huku akifoka na kulia,kilipelekea  wauguzi waje kumnyanyua pale alipokuwa kapiga magoti na kuanza kumtoa nje.

“Niacheni niongee na mama yangu.Nasema niacheni mimi,niacheni.”Binti yule alizidi kung’aka wakati anatolewa chumba kile na wauguzi waliokuwepo zamu.

“Kuna nini jamani?Mbona kelele hivi.Kama sio hospitali bwana.”Aliongea mzee mmoja wa makamo ambaye alikuwa amevalia mavazi nadhifu ya kiuguzi.
“Ni huyu binti anampigia kelele mgonjwa,daktari.”Alijibu muuguzi mmoja aliyekuwa anasaidiana na muuguzi mwingine kumtoa binti yule mule ndani.
“Simpigii mgonjwa kelele,ninaongea na mama yangu.Niacheni tafadhali,niacheni nikaongee na mama yangu.Nawaombeni.”Binti yule aliweka uso wa huruma mbele ya wale wauguzi watatu ambaye mmoja alikuwa ndiye muuguzi mkuu(Daktari mkuu).

“Kama ni mama yake,muacheni akaseme naye kwa njia yoyote. Si mwajua ni mwezi wa tano sasa huyu mama hajielewi hapo kitandani.
 Saa nyingine tutumie njia za kiimani kumponya mgonjwa hasa utabibu wetu unapokuwa unagonga mwamba. Mimi naamini kama mwanaye ataongea,basi mama huyu atasikia hasa mwanaye akiongea kwa upendo. Muacheni akaongee naye,lakini binti usipige kelele, hapa ni sehemu ya wagonjwa, sawa mama?”Muuguzi mkuu alitoa ruhusa na mara moja binti yule aliachiwa huku akimshukuru kwa kumpigia magoti kwa kumfanya arudi tena na kuongea na mama yake.
******
“Samahani mama kama nimekukosea. Nisamehe kwa lililotokea.”Binti yule aliomba msamaha huku akifuta machozi na kamasi chache alizokuwa amezitoa wakati anaongea na mama yake pamoja na pale wauguzi walipokuwa wanamtoa nje ya chumba kile.

“Nakumbuka ulinifundisha kuomba msamaha pale ulipohisi nimekosa. Siwezi kuacha hii tabia ya kuomba msamaha kwani ndiyo imetukuza mimi na wewe pale baba alipotufukuza kwa ukali katika nyumba uliyodumu nayo kwa miaka kumi na sita kama mke wake. Kwa sababu hiyo,siwezi kusema alikufukuza kwake bali alitufukuza nyumbani kwetu.
Lakini sababu gani baba alitufukuza nyumbani kwetu? Ni swali ambalo sikulipatia jibu hadi pale niliposikia ameondoka duniani.

Siku ile kama unaikumbuka vizuri,ulizipata taarifa za kifo cha baba asubuhi na mapema. Wewe kama mkewe uliyefunga naye ndoa halali kanisani,ulijifunga kipande cha kitenge kikuu kuu lakini kwako kilikuwa ndicho kina afadhari. Ulinikamata mkono wangu wa kulia, na moja kwa moja safari ya kwenda nyumbani ikashika hatamu baada ya miezi nane tangu tufukuzwe na baba.

Ulipofika pale wengi walikunyooshea vidole vya mashaka pamoja na visununu ambavyo vilionekana wazi vikitawala katika nyuso zinazoelezea nyoyo zao.
Hukuwajali bali ulijali kuwa unaenda pale msibani kama mke halali wa marehemu,mke mwenye uchungu na mume aliyeishi naye kwa miaka kumi na sita.
Uliniacha pale nje na wewe uliingia ndani ambapo ndipo baba alikuwa amehifadhiwa. Sijui kilichotokea ndani,ila baada ya dakika kadhaa,ulitolewa kwa nguvu na wanandugu wa upande wa baba yangu,Mzee Ched Tambo.
Namkumbuka baba yangu,na nimeshamsamehe. MUNGU akurehemu.”Binti yule iliinama kwa muda kama mwenye kusali kabla hajaamka na kuendelea kuongea na mama yake.

“Sijui wale ndugu wa baba walikuwa na akili gani hadi wakafikia kusema wewe ndiye umeroga baba. Hivi ni kweli kabisa wewe ndiye ulimroga au yule mwanamke wake mpya ndiye alimpa sumu? Hilo swali sijawahi kukuuliza kama unalijua au hulijui,ila nafahamu unajua nini kiliendelea sema ulifunika kombe ili mwanaharamu apite.
Mama mbona mimi sijawahi kukuona ukijishughulisha na mambo ya kishirikina? Mbona  katika makuzi yangu,sijawahi kukuona ukishika tunguri au hata kuvaa kishirikina ni kwa nini wale wakina shangazi na baba zangu walikutuhumu kwa hilo? Au walijua kuwa wewe ndiye utakuwa mrithi wa mali zile na ndio maana walikuchafua? Kwa nini walifanya vile?

Ni maswali ambayo huwezi kunijibu hata kama ungekuwa waweza kuongea. Lakini mimi ninamajibu yote. Najua wao ndio walipanga kifo cha baba yangu wakishirikiana na yule mwanamke mpya ambaye ndiye aliyemchanganya baba hadi usiku ule wa manane akatufukuza nyumbani.
Ha ha haa,ila mama wewe ni jasiri sana.”Binti yule alicheka kidogo kwenye maongezi yake kabla ajaendelea kusema na mwili wa mama yake ambao mapigo ya moyo yalikuwa yanadunda kwa taratibu sana kwa jinsi ile sauti iliyotoka kwenye mashine ya mapigo ya moyo pale hospitali ilivyokuwa inaonesha.

“Unajua kwa nini nimecheka? Nimekumbka usiku ule kabla hatujafukuzwa pale nyumbani. Ulimkunja baba shati lake,na alipoanza kukuletea matusi ulimchapa vibao kama mtoto mdogo. Japo nilikuwa nagugumia maumivu kwa lile teke alilonipiga baba,ila nilishuhudia ukitoa adhabu ile bila kujali yule ni mwanaume na ni mume wako,tena ni kichwa cha familia.
Sikusifu kwa kumpiga,heshima yangu kwake itabaki kama baba. Ila nakusifu kwa kunitetea hasa baada ya mimi kuja kukutea wewe. Japo nilikuwa sina uwezo wa kumfanya baba chochote,lakini nilikupa mwangaza kiasi chake ni nini ulipaswa kufanya baada ya kuona mimi napigwa kwa sababu nakutetea.”Maneno mazito yaliendelea kutoka mdomoni mwa binti yule na wakati huo yule muuguzi mkuu ni kama alivutwa sana na ile historia ya uchungu kutoka kwa mwana kwenda kwa mama.

”Baba alikuwa amelewa na ndio maana uliweza hata kumpiga mitama na akasaliti amri,lakini kama angekuwa hajalewa siku ile ningeshuhudia mpambano wa ajabu sana,na katika kuepuka hilo ili lisije kutokea,uliamua kunichukua usiku uleule huku matusi ya baba yakitufuata,tukaondoka pale nyumbani. Kila kilichokuwa chetu kwa usiku ule,baba alishiriki kuturushia kwa kuwa alikuwa anavimiliki yeye katika chumba chake.

Tuliondoka pale huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha bila kukoma wala kupumzika. Ilikuwa ni mvua hasa. Mvua ambayo iliishia mwilini mwetu.
Sikujua tunaenda wapi lakini safari yetu iligotea mbele ya nyumba moja kubwa. Nyumba ambayo sikuweza kuitambua hadi pale tulipofunguliwa na mwenye nyumba ambaye kwa haraka niligundua ndiye mwenyekiti wa ule mtaa.

Hakutaka tusogelee nyumba yake hata tusimame pale ambapo hapakuwa na mvua. Kwa kuwa yeye alikuwa na mwamvuli,basi hali ya kulowa kwetu yeye hakuitambua maumivu yake. Namkumbuka yule mzee,namkumbuka vizuri sana. Sijasahau sura yake,sauti yake kali iliyotufukuza kwake na wala sijasahau jina lake maarufu pale mtaani,aliitwa Mzee Michanga.”Binti alipofika pale alimeza mate ya uchungu kisha akaendelea kuelezea kilichotokea.
  
“Yule Mzee Michanga ujue niliona kama utani pale alipotukatalia kwenda kusimama pale kibarazani ambapo tungejikinga na mvua na kumuelezea shida yetu. Ilikuwa kama utani kweli na mimi nilidhani anatania kwa jinsi mzee yule alivyokuwa ananipenda na kunitania japo nilikuwa sipajui kwake.
Ila nilishangaa ule utani umemuisha wote,alitufukuza kama mbwa pale kwake. Au siyo kama mbwa,alikuwa anatufukuza kwa kutusukuma kama wafanyavyo askari waliyomkamata kibaka ambaye anagoma kwenda kituoni.

Yule mzee alitutoa nje huku bado mvua na baridi vikiendelea kutusakama miili yetu kana kwamba vilitumwa kwa ajili hiyo,na mvua ya Sumbawanga pamoja na baridi yake,siku ile ningesipobanwa na pumu,ningesipoumwa tena na na gonjwa lile. Ugonjwa ambao umetibika baada ya mimi kufanikiwa kimaisha,juzi tu hapa ndio nimetibiwa baada ya mume wangu kunipeleka hospitali moja kule Uholanzi.
Hizi ni taarifa nzuri kwako mama,najua huwezi kuamini hasa ukiikumbuka siku ile.”Binti yule wa miaka ishirini na nane aliongea hayo kwa faraja huku akishika nywele za mama yake na muda mwingine kuzilaza.
Bado yule daktari alikuwa kaegemea katika mlango huku akiwa makini kufatilia yale maneno ya yule mwanadada. Dada ambaye kimuonekano ni kama alikuwa hajapitia yale maswahibu yale. Alikuwa ni nadhifu pamoja na kujiweka kama wasichana wa kileo.
Daktari akawa anaendelea kuyaingiza akilini maneno yaliyojaa uchungu mkubwa toka kwa mwanadada yule.

“Tulifukuzwa pale,usiku uleule na mvua ikiwa inanyesha. Ulininyanyua na kunibeba kisha ukaanza kukimbia kulekea palipo salama,na wakati huo huku nyuma yule Mzee alibamiza geti lake na kuingia ndani.
Safari yetu iliishia kwenye kibanda kimoja cha makuti kilichopo pale mtaani kwetu,kibanda ambacho kiliponipokea,nikaanza kuumwa palepale.
Kifua changu kikaanza kunibana bila kunipa nafasi ya mimi kupumua. Licha ya mengi yaliyotukia nyuma,ila pale ndipo nilidhihirisha kuwa uchungu wa mwana,aujuaye ni mzazi.” Mwanadada aliinamia godoro la hospitali na kutoa chozi la uchungu lakini alipoamka hakuacha kuendelea kuongea alichokusudia.

“Nikiwa na umri ule wa miaka saba ndani ya kibanda kile kidogo cha makuti tena mvua na radi zikizidi kupamba moto huku nje, kifua kile kilichosababishwa na pumu, kilinifanyaa ndani ya sekunde kumi nitoe pumzi moja tu!
Nilikuwa sijielewi,ni kama nilipoteza fahamu lakini bado nilikuwa nauwezo wa kusikia na kuona,lakini akili ililala kabisa. Najua mama ulihaha huko na huko kutafuta tiba lakini ulichoambulia ndicho kilichoniponya.Yale masarufeti uliyoyafanya kama kitanda changu, pamoja na zile nguo chache tulizotoka nazo nyumbani ambazo baadhi zililowa,ndizo zilikuwa mashuka yangu.
 Hukuishia hapo mama,kwa upendo wako na uchungu juu yangu, ulitoa gauni  lako ulilokuwa umelivaa ili ukinigusana nalo nisisikie baridi kwa kuwa lililowana. Ukalitupa pembeni na kunikumbatia ili uongeze joto katika mwili wangu,nani kama wewe mama? Ni nani kama wewe? Amka mama,tafadhali amka.”Dada yule aliongea kwa uchungu uliojikita moyoni mwake hadi ule mwili wa mama yake ambao ulikuwa haujawahi kutikisika kwa miezi mitano mfululizo,safari hii ulitikisika.
Naam,kidole chake cha shahada kilitikisika na hata daktari mkuu aliona lile. Maneno ya mtoto yalimuingia mama,sasa akawa anapigana japo aweze kumuangalia mwanaye aliyeteseka naye kwa nusu ya maisha yake.

Daktari alitoka pale mlamgoni na kumfuata yule mwanadada na kumshika begani.
“Binti endelea.Mama anapigania  nafsi yake ili akuone. Endelea ulichokianza,usilie sana mwanangu.”Daktari yule wa miaka kama sitini,alimfariji dada yule.

“Dokta,hivi wajua ndugu yako wa kweli ni yule ambaye mmechangia damu ya wazazi na si yule uliyeunganika naye kutokana na mke au mume wako kuwa pamoja? Hapa na maana kwamba,ndugu wa mke wako si ndugu zako wewe. Kama uamini, basi subiri mkeo aondoke duniani uone kama watakuthamini hasa pale ambapo utakuwa huna kitu.
Sisemi haya kama nakutisha au kukukanya au kukujaza fikra zangu,bali nasema haya kwa kuwa nimepitia maisha haya,na nimeona kwa wenzangu pia wakiyapitia. Kwa hiyo namaanisha kwa ninachokisema.”Mwanadada yule alimgeukia daktari mkuu wa hospitali ile na kumwambia maneno haya ambayo kwa daktari yawezekana yalikuwa mapya au yalikuwa kama nyongeza katika kujifunza kwake.

“Mama yangu ujue alitolewa na wale wanandugu nje ya chumba kile kilichohifadhiwa maiti na kuambiwa yeye ndiye kamroga baba. Na vile vidole ambavyo vilikuwa vinatulenga wakati tumefika pale,vilikuwa vinatulenga kwa ubaya.
Nasema vilitulenga kwa ubaya kwani pale mama alipobwagwa nje na wale ndugu wa baba,mara vidole vile viligeuka na kuwa midomo.
Wale waliyotuoneshea vidole,wakasimama kishughuli  zaidi.Kila neno chafu ambalo waliona sawa kulitupia kwenye himaya ya mama yangu,walilitupia bila kumuonea huruma. Ni kama walishajazwa ujinga wale watu wa kule. Waliamini mambo ya kishirikina kuliko MUNGU,sijui ni watu wa aina gani na sijui wataelimika lini.

Wanavyosema eti walienda kwa mganga ndipo yule mganga akasema mama yangu ni mchawi na ndiye kamroga mume wake kwa kuwa baba alitufukuza pale nyumbani. Hivi kweli hata wewe dokta waweza kuamini hilo? Waweza kukubali kuwa mama yako ni mchawi na wakati kaishi mumewe miaka kumi na mitano bila mumewe kutoa maneno hayo.Kweli kabisa,waweza kuamini hilo dokta?”Maneno yanayoweza kumtoa yeyote machozi yaliendelea kutolewa na dada yule mrembo.
Dokta alikuwa mtu wa kutikisa kichwa kushoto na kulia kama mwenye kusikitikia yale ambayo yalikuwa yanamtoka binti wa miaka ishirini na nane. Binti ambaye alikuwa sawa kabisa na binti wake wa pili.

“Nyamaza mwanangu. Hayo yote ni mapito tu! Sidhani kama nikikwambia hakuna marefu yasiyo na ncha,utakataa usemi huu kwa kuwa sasa ulishavuka hayo yote. Kinachokuangalia kwa sasa ni uhai wa mama yako. Ni wewe uliyeweza kufanya kiungo chake kimoja kitikisike,naamini ni wewe pia ndiye utafanya hata mdomo wake uongee,macho afumbue na mwili wake usimame wima kwa ajili ya kuendeleza mapambano ya maisha haya.”Daktari aliongea kiushauri zaidi na kumfanya yule dada amuangalie mama yake pale kitandani akihemea mipira.

“Hukuwa hivi mama. Hukuwa mtu wa kuhemea mipira kama gari au mashine ya kunyonyea mafuta. Hukuwa hivi mama,hukuwa hivi kabisa. Hukuwa mtu wa kulala muda mrefu hivi bila kusema chochote. Sikuwahi kukuona umeamka saa moja asubuhi bali muda wako ulikuwa ni saa kumi na moja au saa kumi mbili. Yote hayo uliyafanya ili kuhakikisha unatafuta chochote kwa ajili ya maisha yetu. Na ulifanikiwa hilo mama yangu.
Hata siku ile nilipobanwa na pumu usiku,hukuweza kulala kwa raha na hata ulipolala sidhani kama ulikuwa unaota kitu kingine zaidi ya maisha yangu. Sijui nikufananishe na nani,wewe ni mama wa aina gani? Ni mwadamu gani wewe mama?
Ni mwanadamu gani ambaye anaweza kufurahi nilipodai chakula baada ya usiku ule wa ugonjwa wangu kupita? Nilidai chakula mimi kana kwamba pale nilikuwa nyumbani na kumbe tulikuwa kwenye kibanda kilichotuhifadhi kwa muda tu!
Lakini wewe hukujali hilo. Nilipokuamsha kwa sauti chovu na kukwambia nahisi njaa. Wewe ulitabasamu na kunikumbatia huku ukilia na kuniambia ulidhani nitakuacha mpweke.
Nisingeweza kukuacha mama yangu. Naomba na wewe usiniache. Amka mama,tafadhali amka.”Safari hii wakati dada yule anaongea,chozi lilimtoka yule mama kwenye jicho lake la upande wa kushoto.
Ama hakika ilikuwa ni muujiza,hata daktari alishindwa kuvumilia na akajikuta akitoa chozi  baada ya kuona mama yule anatoa chozi ambalo hakuwahi kufikiria kama itakuja kutokea kwa kitu kama kile. Mama yule alikaa kwa muda mrefu sana pale hospitali,hiyo ndio sababu ya hata daktari kutoa chozi lake ambalo naweza kusema lilikuwa ni la furaha.

“Kila mara ulitoa chozi kwa sababu yangu. Naamini hata sasa unafanya sawa na kile nachokiamiani. Umetoa chozi  kwa sababu una uendo juu yangu. Nami nakupenda sana mama,ila nakuomba uamke ili nikuoneshe upendo huo.”Huruma na huzuni iliendelea kutawala ndani ya chumba kile cha wagonjwa walio mahututi kutokana na maneno aliyoyatoa binti yule.

“Ulitoa chozi la uchungu pale ndugu wa baba walipokupora na kunichukua mimi ili niishi nao kwa kusema eti mimi nilikuwa damu ya baba na si yako. Ulinililia sana nakumbuka. Sikuwa nyuma kulia pia,nilikulilia huku nanyoosha mkono unikamate,lakini haikuwezekana. Walikuwa wamekamata vizuri tayari kwa kunipeleka ndani na kunifungia huko.
Nachojua walikufukuza pale msibani na hata kwenye mazishi hawakutaka kukuona kwa ahadi ya kuwa kama ungeenda,wangekumaliza.”Mate mazito na ya uchungu yalipita kooni kwa mwanadada yule kabla hajaendelea kuongea aliyoyaanza.
*****
“Baada ya mazishi ya baba.,maisha yalianza upya. Mimi nikiwa nalelewa na mama wa kambo na pale nyumbani akiwepo baba mdogo tukiishi naye.Hiyo ni baada ya kukaa kikao cha familia,maamuzi yao yalikuwa hivyo. Hawakukuzungumzia wewe hata kidogo.
Nashukuru baba mdogo alikuwa ananijali sana. Shule alinianzisha na kila nilichokiomba alinipatia. Ila tatizo lilikuwa kwa huyu mama yangu wa kambo. Huyu ndiye chanzo cha mimi kujua kuwa baba aliwekewa sumu katika chakula, na ni huyu huyu ambaye alitaka kuniua na mimi na ndio maana nilikutafuta usiku na mchana ili nirudi kuishi na wewe. Nisingeweza kukaa na yule mama muuaji.” Dada yule aliendelea kuongea kwa masikitiko huku sauti yake ikijaa kilio kikubwa ambacho ni MUNGU pekee ndiye awezaye kupima ni kiasi gani kilikuwa kina maumvu.

“Najua hujui hili,na sina nia ya kukuumiza zaidi. Ila kuna siku Baba Mdogo na Mama walikorofishana ndipo nilipopata  ukweli wote kuwa baba alilishwa sumu na mimi nilikuwa nafuata kulishwa ,nilisikia haya kwa masikio yangu na ndipo nilichukua hatua ya kutoroka na kuja kwako. Hakika mama  nakwambia,nilichukua zaidi ya wiki tatu kukupata ulipo. Nilipita kila njia ilimradi nikuone. Mvua na baridi viliutawala mwili wangu kuliko dunia hii.
Hadi nakuja kukupata,kweli nilikuwa nimehangaika lakini nashukuru MUNGU nilikupata, sina cha kumlipa Mola wangu zaidi ya kuzidi kumwomba.”Safari hii binti alishusha uso wake wa huzuni kwa kuangalia chini,na pale alipounyanyua,alikuwa katengeneza tabasamu hafifu lakini lenye imani na likifanyacho.

“Hivi mama unakumbuka tulivyotoka pale Mpanda Mjini na kwenda kuanza maisha ya kijijini kule Sitarike(Kijiji kilichopo Mpanda)? Kule ndipo bahati yangu ilipoanzia. Na hadi leo nina miaka ishirini na nane lakini nakumbuka sana bahati ile. Nawakumbuka wazazi wa mume wangu na namkumbuka mume wangu pia tangu udogo wake.”Dada yule aliongea huku tabasamu lake likizidi kadiri alivyoendelea kuongea.
“Daktari, hivi waweza kuamini kuwa  mvulana niyekutana naye miaka kumi na tisa iliyopita,tena nilikuwa namuona kwa mwezi mara tatu. Halafu baadaye akapotea kabisa maishani mwangu. Akaja kuibuka tayari mtu mzima na mwenye maisha yake, eti leo ndio kanioa. Mwanaume ambaye sikuwahi kumfikiria maishani mwangu kuwa tutakuja onana kutokana na yeye kutokea nchi za ughaibuni,leo hii ni mume wangu na tuna watoto. Amka mama uwaone wajukuu zako,amka mara moja tu! Uwasalimie,huu ndio ujumbe niliokuletea kwako  leo hii.”Sura ikiendelea kutawaliwa na tabasamu pamoja na huzuni,iliendelea kumtaka mzazi wake azinduke.

“Najua wajua ni bahati gani niliyokuwa nayo mwanao,ila leo nakukumbusha tu. Pale tulipohamia Sitarike,ndipo nyota yangu ilipoanza kung’aa.

Nikiwa nina miaka tisa, sikujua kutofautisha kati ya raha na shida katika maisha yangu ya utoto. Hata watu walivyosema sisi tuna shida, mimi niliona kama wananitania tu!maana maisha niliyoishi hadi muda ule yalikuwa hayana tofauti sana na yale niliyozaliwa nayo. Tofauti yake ilikuwa ni mdomo wa mama.Wakati ule wa miaka mine hadi saba, mama alikuwa ananibeba na kunibembeleza lakini muda ule alikuwa ananibeba kwa kunihasa na kunibembeleza kwa ushauri, kipindi hicho nilikuwa na miaka kumi.
Mungu kaniumba na bahati pamoja na kipaji,hilo nitasema daima.Ila Mama ulinikomaza kiakili ili nikitumie kipaji na bahati zitakazokuja maishani mwangu. Na kama kweli Mungu hamtupi mja wake, basi hakunitupa mimi.

Nikiwa na umri ule wa miaka kumi,nilibahatika kupata marafiki wa Kizungu ambao walikuwa wanapenda sana kutembelea hifadhi ya Katavi. Mara ya kwanza kuja, walikuwa kama wamepotea na ndiyo maana wakawa pale Sitarike.”Mwanadada alimeza mate kisha akaendelea kuhadithia.

“Wakiwa na mkalimani wao wa lugha ya Kiswahili, waliomba niwaoneshe Katavi ilipo,na mimi kwa uzoefu wangu nikawapeleka hadi huko wanapo pataka. Hapo ndipo kidogo nilianza kujua tofauti ya raha na shida.

Ikiwa mara yangu ya kwanza kupanda gari tangu nizaliwe,niliona maajabu ya mtoto kulilia kitu na kupewa mlemle kwenye gari. Kwa mara ya kwanza tangu afariki baba,nikaonja chokoleti niliyopepewa na yule mtoto wao wa Kizungu.Na mimi siku hiyo,mbona pale kijijini walinikoma,kisa nimekula chokoleti.”Tabasamu na cheko dogo lilimtoka yule dada baada ya kusema hivyo,pia alimuangalia muuguzi mkuu naye alikuwa kachanua tabasamu la furaha usoni pake. Dada yule akazidi kuendelea kusimulia.

Nilikuwa Mwalimu wao kwenye ile hifadhi zaidi ya hata wale wanaojiita wamiliki.Niliweza kukaa na simba hata kama ajapigwa sindano yenye dawa ya usingizi. Walinipenda sana,na kila walivyokuwa wanakuja,walikuja na zawadi kwa ajili yangu. Wakawa wananipa hela nyingi sana ambazo mama ulizihifadhi vizuri kwenye pochi yako maalum kwa ajili hiyo.

Lakini baada ya miaka miwili, ndipo nikaamini kuwa kisicho ridhiki hakiliki. Sababu ya hila za binadamu na visununu mioyoni mwao, wazungu wale walisimamishwa kuja katika hifadhi ile na hifadhi yeyote Tanzania kwa sababu ambazo zilikuwa hazina vigezo ya kuitwa sababu.
Wazungu wale waliitwa wezi wa wanyama wadogo wa hifadhi wanazotembelea, na waliwaiba kwa kushirikiana na wafanyakazi wa hifadhi hizo.

Lakini kiukweli, hawakuwahi kufanya hivyo katika macho yangu hata mara moja na mimi nilikiwa mmoja wa kuwatetea wale wazungu. Sheria ilisimama mahala pake na panga lake likawapitia. Huo ndio ukawa mwisho wa wale wazungu kuja Tanzania.” Kimya kikatanda kidogo kabla binti yule hajarejesha uso wake machoni kwa mama yake na kuendelea kuelezea maswahibu ya maisha waliyopitia.

“Japo waliondoka,lakini waliweza kutuachia fedha nyingi ambazo zingekidhi mahitaji yetu. Na ndipo hapo ulipoamua uhame na mimi na kuja huku Dar es Salaam.
Huku ulifanya shughuli ndogo ndogo ili maisha yaende. Ukanipeleka shule kwa zile fedha kiasi na namshukuru Mungu kwani mama yangu ulikuwa na amani kupita kiasi, na yote uliyofanya yalikuwa kwa ajili yangu mama. Hakuna kitu nachokipenda duniani kama Mama yangu,nakupenda mama. Amka basi nikuoneshe upendo huo,amka ili uone ndoa yangu mama.”Kilio kilianza tena kwa dada yule
Muuguzi alichukua jukumu la kumfariji mwanaadada yule kwa kumpigapiga na kumsugua begani kitu kilicholeta faraja tena kwa binti yule.

“Asante daktari. Asante sana.”Shukrani zilimtoka mwanadada kumwendea daktari mkuu aliyekuwa anaendelea kusikiliza kisa na mkasa wa mwanadada yule.

“Nilisoma kwa bidii sana tena sana. Na mwisho wa siku nilimaliza kidato cha nne na kufaulu vizuri tu. Sasa tatizo likawa fedha ya kuendelea na kidato cha tano na sita. Hapo suala la kuendelea na elimu likagota. Nikashindwa kuendelea kwa kuwa sina fedha hizo.
Ikanibidi nikae nyumbani na kusaidiana na wewe katika biashara. Na ninashukuru sana kwani biashara ilitanuka zaidi na zaidi hadi tumaini la kuendelea kidato cha tano na sita likafufuka. Hiyo ni baada ya miaka miwili ya mimi kumaliza kidato cha nne.

Lakini ya MUNGU ni mengi sana. Unaweza kupanga hili,likatokea hili. Na ndicho kilichotokea. Wakati tunapanga nirudi darasani,mara mama yangu mpendwa ukaugua. Uliugua sana nakumbuka,lakini ulipigana na kunyanyuka tena. Nakuomba upigane na hapa pia,amka mama yangu. Jitahidi kama kipindi kile,amka mama.”Huruma ikazidi kutawala chumba kile cha wagonjwa mahututi lakini faraja ilikuwepo kwa mama yule kuamka, kwani hata kile kifaa cha hospitali kioneshacho na kutoa sauti ya mapigo ya moyo yanavyoenda,kilizidi kupanda na kufikia pointi ya matumaini japo bado haijawa sawa kabisa.

“Endelea binti. Endelea. Mama atarudi katika hali yake.”Daktari alijaribu kumpa moyo mwanadada huku mkono wake ukimgonga gonga bega.
Mwanadada alimuangalia daktari kwa jicho la huzuni,kisha akarudisha macho kwa mama yake. Ni kama alikuwa anayapima maneno ya daktari yule kwa kuangalia hali ya mzazi wake. Mipira puani na mdomoni,macho yamefumbwa na haja zote zinatoka palepale,ni kweli ataamka?
Maswali kama hayo yalipita kichwani mwake,lakini alipiga moyo konde na kuendelea kusimulia.

Nilikuwa na miaka ishirini na mbili kipindi kile. Naikumbuka siku ile ya ugonjwa wako.
Ilikuwa ni usiku mnene,mtaa wote ulikuwa kimya.Mara mama uliugua ugonjwa ambao sikuujua hapo kabla hadi wataalamu waliposema ni tetenasi iliyosambaa mwili karibu wote.Hakika mama nilipagawa kwa taarifa hiyo. Nilihisi kutaka kukimbia hasa baada ya kujua athari za ugonjwa ule.

 Mbaya zaidi,ni palewalipotaja  gharama za kuitoa sumu hiyo pamoja na matibabu mengine,ilikuwa ni zaidi ya milioni mbili na wakati huo tulikuwa na laki tatu pekee za mtaji wetu.Hakika mama nilichanganyika,nilichanganyikiwa sana hasa pale nilipokuangalia. Ilikuwa kama hivi,lakini madaktari walinifariji kuwa utapona kama gharama zitalipiwa.

Nilipokuangalia mama yangu,ulikuwa umeganda tu kitandani,sijui kama ulikuwa wajua dunia inaendaje wala sidhani kama ulijua ni kiasi gani moyo wangu ulivyokuwa umejeruhiwa kutokana na hali yako.

 Nilirudi nyumbani na kuuza kila kitu ili mama upone,sikujali nitakula nini mbele wala nitaishije. Nilichojali ni wewe kurudi katika hali yako.Wewe ni kila kitu kwangu.

Nikafanikiwa kupata milioni moja ambayo niliilipa kwa matibabu ya mwanzo. Kidogo mama ukapata nafuu na uliongea huku unatoa chozi ambalo safari hii halikuwa lile la kuniona nimeamka na kudai chakula bali la maumivu ya jinsi navyohangaika kwa ajili yako.
 Na sasa bado naendelea kuhangaika ili unyanyuke. Amka mama yangu,nakuhitaji,tafadhali amka.”Kilio cha kwikwi kikafuata huku mikono ya dada yule ikalifinya shuka la hospitali kutokana na uchungu uliomjaa moyoni.

“Binti pigana. Endelea kupigana mama aamke,usilie. Mama anakusikia,endelea kumuamsha,ataamka tu.”Sauti nzito ilibembeleza kilio cha mwanadada na kweli ilifanikiwa a dada aliendelea kuongea.

“Ulichofanya ni kunihasa na mambo ya dunia sana. Nilikusikiliza yote uliyoniambia,sikutaka kuacha hata chembe ya neno lako kunipita. Na ninakumbuka ulinikataza nisitoe chozi hata moja kwa lolote lile japo wewe uliongea hayo huku  wafanya hivyo.”Sauti ya mwanadada yule iliendelea kutoka kwa simanzi huku ikikosa faraja ya mtu inayomwambia.
“Kumbuka haya maneno mama,nilikwambia wakati u maututi.”Alimeza mate kidogo kisha akamkumbusha maneno ambayo aliwahi kumwambia mama yake baada ya mama yake huyo kumuhasa sana kuhusu maisha na kumtaka asilie pale chochote kikitokea.Mwanadada alisema haya kwa mama yake,

“Usijali mama, kwa uwezo wa MUNGU utapona na haya yote utaniambia nikiwa nimelala miguuni mwako".
“Niliongea hayo huku nakufuta machozi yako kwa giganja changu cha mkono wa kulia.
 Ulinishika kichwani na kuniinamisha hadi usoni kwako na kunibusu shavuni kuonesha upendo wako kwa kijana mimi ambaye ndiyo kwanza nilikuwa naanza kuyajua maisha.
Nakumbuka mama busu lile la faraja,nalikumbuka sana. Tafadhali,amka mama,nalihitaji busu lako tena,amka mama.”Bembelezo la machozi liliendelea kutinga katika chumba kile huku matumaini ya mama yule yakiwa hafifu katika moyo wa mwana wake.
******
 “Dokta.”Safari hii ilimgeukia daktari mkuu mwenye dhamana ya kumuangalia yule mama hadi apone. Baada ya kumuita na daktari kuonesha umakini wa kuitwa kule,alianza kumsimulia  kilichoendelea katika maisha yao.

“Hali ya mama ilibadilika tena baada ya wiki moja,tena tukiwa palepale hospitali. Nikiwa sijui cha kufanya kwa sababu sina kitu nilichobakiza,ndipo Daktari aliniambia inatakiwa milioni moja na nusu ili mama apone kabisa maana zile dawa na matibabu aliyopewa kwa ajili ya kumpa nguvu tayari zimeshindwa kuendelea kufanya kazi kwa kukosa ushirikiano wa vitu muhimu hasa chakula bora.

Kwa maneno hayo ya daktari mwenzako,unadhani ningetoa wapi fedha hizo alizihitaji? Na hakuishia hapo, aliendelea kuniongezea uchungu zaidi ya mwanzo.”Mwanadada aliongea hayo kama kumfikishia ujumbe daktari. Akaendelea,

“Daktari aliongeza kuwa nina siku nne za kuleta hela zile ili mama yangu apone. Mama akiwa hajitambui kabisa pale kwenye kitanda cha hospitali,na  huku mashavu yake yakiwa yametengeneza michirizi ya machozi ambayo alikuwa analia sababu yangu, nilimuaga kwa kumuambia nitarudi baada ya siku tatu.
Sikujua naenda wapi wala sikujua naenda kufanya nini kwa wakati ule,ila nilichojua ni kwamba naenda kumsaidia mama yangu ili apone.

Huwezi kuamini Daktari. Hii dunia wema ni wa kuwahesabu,na hadi uwapate yakupasa kupamana hasa. Mimi sikupata mwema hata mmoja katika tafuta zangu. Wale rafiki ambao nilidhani watanielewa nikiwafuata,walikuwa kama nyati aliyejeruhiwa pale nilipowafuata. Walikuwa wagumu kuliko chuma na wenye wingi wa maneno yasiyokuwa na msaada kwangu.

Achana na hao marafiki. Kuna wazee wengine ni wa heshima kabisa. Familia zao zinawategemea katika kutoa ushauri. Na wengine ni viongozi wa dini na serikali,lakini mambo waliyoyataka,kiukweli sitaomba tena shida zinikute.
Kwa kuwa nilikuwa namsaidia mama yangu,ilinibidi niuze hata mwili wangu ili mama apone. Ndiyo, niliuza mwili wangu kwa hawa wana…...”Aliposema maneno hayo mara hali ya mama yake ilibadilika na kuwa tofauti na mwanzo.
Kile kipimo cha mapigo ya moyo kiliongezeka kasi kitu kilichoonesha mapigo ya moyo pia yameongezeka kugonga katika kifua cha mama yule.
Macho pia yalifunguka huku midomo yake ikitaka kuongea lakini ilishindwa kutokana na mipira iliyokuwa imeingia kinywani mwake kumzuia. Pia pumzi iliyokuwa ikitoka kwa shida hapo nyuma,sasa uliongezeka na kuwa kama ya mtu anayekimbia umbali mrefu,jambo ambalo lilimfanya Daktari kutoa kile kifaa kilichokuwa kikimsaidia mama yule kumpelekea gesi ya oksijeni.

Daktari alikuwa kama haamini kinachojiri kwa wakati ule. Aliwaita wauguzi wenzake ili waje kumsaidia kumuondoa katika chumba kile na kumpeleka chumba ambacho wataweza kuondoa vile vifaa vilivyokuwa vinamlisha na kumpa pumzi.

Ni kitendo kilichochukua nusu saa. Tayari mama yule alikuwa katolewa vile vifaa na kupelekwa wodini ambapo hakukuwa kule kwa wagonjwa mahututi bali kwenye wodi ya kawaida.

“Veronica.”Daktari mkuu wa hospitali ile alimuita yule dada aliyekuwa anaongea na mama yake ambaye kwa jina sasa alijulikana kama Veronica.

“Mama anakuita.”Daktari alipeleka ujumbe huo baada ya Veronica kuinua kichwa pale alipokuwa amekaa na kumuangalia anayemuita.

“Hapana Dokta. Mama kajua kuwa niliuza mwili wangu ili atibiwe. Sitaki kwenda kumuona,naogopa sana Dokta. Nitamuangaliaje leo hii?.”Veronica alionesha wasiwasi wake hasa kwa kitu alichokifanya miaka sita iliyopita.

“Mama anakuita Vero,nenda kamzikilize. Ulitaka aamke,sasa ndio kaamka,yakupasa kwenda na kumsikiliza anachokuitia.”Daktari alimsihi Veronica,naye Veronica alinyanyuka pale kitini alipokuwa amekaa na kumfuata Daktari anapoelekea.
******
“Vero mwanangu. Njoo mwanangu,njoo karibu. Nimeamka mama yako.”Mama yule aliongea kwa sauti ya chini huku akiunyoosha mkono wake kumuelekea mwanaye ambaye alikuwa akisitasita kwenda.

“Tafadhali njoo mwanangu. Hujafanya chochote kibaya. Usiogope.”Mama yule alikuwa kamaameusoma moyo wa Vero hivyo Veronica alisogea alipkuwa kalala mama yake na kumkumbatia kwa nguvu ikifatiwa na sauti ya kilio iyotawala kwa muda kiasi kabla ya Doktari kuingilia kati na kuwasihi wasifanye vile kwa manufaa ya mgonjwa ambaye alikuwa hajapona kabisa kutoka katika hali yake.

“Umeamka mama yangu. Asante sana MUNGU kwa kumrudisha mtu nimpendaye katika maisha yangu. Asante sana MUNGU.”Veronica aliongea hayo huku akiangalia angani  akiwa na imani kuwa MUNGU alikuwepo huko.

“Nimerudi kukupooza mwanangu.Nisingevumilia hali uliyokuwa nayo baada ya mimi kuondoka. Nimepigana ili kuinusuru roho yangu kuondoka bila kuwaona wajukuu zangu na ndoa yako. Nakupenda sana Vero.” Mama yule aliongea huku akiwa kaweka tabasamu hafifu lakini lenye matumaini.

“Dokta.”Veronica alimuita Daktari ambaye alkuwa kasimama pembeni huku tabasamu la haja likiwa limetawala usoni mwake.
“Naam binti yangu.”Daktari aliitika.


“Mama karudi.”Veronica aliongea kwa furaha kisha akamfata Daktari na kumrukia huku pia akimpa kumbate ambalo Daktari alishindwa cha kufanya zaidi ya yeye pia kumkumbatia.
“Hujanimalizia hadithi yako lakini. Ulifanikiwa kupata pesa za kumtibia mama yako?” Daktari aliuliza baada ya kumaliza kukumbatiana na Veronica.
Vero alimuangalia mama yake kama mwenye kumuuliza amuhadithie au asimuhadithie ile hadithi huyu Daktari. Na mama yake aling’amua lile swali la macho,bila hiyana alimpa ruhusa ya kuimalizia ile hadithi.
Vero alizidi kumuangalia mama yake kwa macho ya huruma,na kisha kwa upendo mkubwa, alikaa pembeni yake na kuanza kuongea tena.

“Shida na mateso uliyoyapitia ukiwa nami, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nisiposema asante na MUNGU akupe mwanga zaidi katika maisha yako.
 Mama, asante pia kwa kuniwezesha kuaminika na watu japo elimu yangu yenyewe siyo kubwa ya kuweza kufanya haya ninayofanya sasa hivi. Hakuna kama wewe mama, na ninakupenda sana mama yangu, hilo siwezi kulificha kwa MUNGU hata kwa yeyote yule ambaye atataka kujua kiasi gani nampenda mama yangu.”Alimshukuru mama yake na kisha akamgeukia Daktari.

“Dokta, ni miaka sita sasa imepita tangu lile tukio la mama kuumwa litokee.
Nasema ukweli kuwa sikuamini siku ile nilipoondoka na kutokomea kusipojulikana kisha baada ya siku tatu nikarudi kuja kushuhudia kitakacho kutokea,kwa sababu sikupata ile fedha niliyoagizwa na hospitali.
Mwili wangu ulichezewa lakini haukuweza kufanya fedha ya mama kutibiwa ipatikane.Lakini MUNGU anamaajabu yake,na MUNGU si Athumani Dokta.
 Nilishikwa na butwaa pale nilipofika hospitali na kumkuta njemama yangu anaota jua la jioni, na aliponiona, alinyanyuka na kunikimbilia kana kwamba hakuwa kitandani wiki bila kujitambua.
Hata pale aliponikumbatia, nilihisi ni ndoto bado kama hii ndoto nayoiona sasa hivi.Lakini joto na sauti yake ya msisitizo ndivyo vilivyoamsha hisia zangu na kurudisha furaha yangu tena.
Watu walitutazama jinsi mama alivyokuwa amenidandia mwanae na huku mwana naye kakushikilia vizuri ili msidondoke,najisikia faraja sana mama yangu  kwa lile tendo.”Hapo tena alimgeukia mama yake na kumkuta  kapambwa na tabasamu mwanana usoni pake. Akamgeukia Daktari tena na kuendelea kusimulia.

“Lakini siri ya kupona kwako mama, ni nini? Ni kwa sababu ya wema uliyonifundisha kuutenda tangu utotoni kwangu. Wema wangu niliyoutenda miaka kumi na kitu iliyopita kwa wale wazungu, siku ile uligeuka kuwa dawa yako mama yangu.

Sikuamini kuwa yule kaka aliyelipa zile fedha za matibabu kuwa ndiye yule aliyenipa chokoleti kipindi kile cha nyuma.
 Mtu ambaye alinifanya nijigambe kwa watoto wenzangu pale kijijini kwa sababu ya chokoleti aliyonipa. Leo hii ni mvulana mkubwa na mwenye akili zake za kufanya mambo yake binafsi,na siyo yule wa kulilia tena vitu kwa wazazi wake. Kweli hii ndio dunia bwana.

Kalipa wema wake kwetu japo sikuwahi kumfanyia jambo kubwa zaidi ya kuwazungusha yeye na wazazi wake mbuga za wanyama.Sijajua alilipata taarifa wapi kuwa tupo Dar es Salaam,ila nachojua alitusaidia hadi  mama akawa mzima lakini ugonjwa wake umerudi tena mwaka huu. Na umekuja kwa kasi ya kutaka kumchukua kabisa.
Nakushukuru Daktari na jopo lako la wauguzi kwa uangalizi wenu kwa mama yangu. Sina cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea kwa MUNGU awazidishie kila mtakachomuomba.”Veronica alimaliza kumsimulia Dokta na kugeuka tena kwa mama yake.

“Tumepata watoto mapacha mama na mume wangu mtarajiwa. Nimekuja nao sema nimewaacha nyumbani,utawaona wajukuu wako.”Veronica alimpa taarifa mama yake ambaye alizidi kutabasamu baada ya kusikia hayo.

“Daktari. Yule mzungu aliyenipa chokoleti na kumlipia mama gharama za matibabu,ndiye mume wangu mtarajiwa,nilikuwa naishi naye Uholanzi. Mimba niliyokuwa nayo,nikashauriwa nisisafiri umbali mrefu kwa sababu ya afya yangu.
Maisha ndivyo yalivyo Daktari. Huwezi jua wema wa leo utaleta fadhila lini. Tenda wema,fadhila zitakuja pale usipopategemea.”Vero alimaliza kwa ushauri mdogo kwenda kwa Daktari aliyemtibu mama yake.

Alimuangalia mama yake na wote wakajikuta wanacheka cheko ya pamoja ambayo Daktari alishindwa kuitafsiri bali alisubiri vicheko vile viishe ndio aulize. Lakini haikuwa hivyo,mtu na mwanaye walipomaliza kucheka,mara moja wakampa jibu Daktari juu ya vicheko vyao.

“Na wewe unajidai umekuwa mtu wa ushauri eeh, embu lione kwanza.”Mama Vero aliongea hayo akimtania mwanaye.

“Wewe ndiye uliyenifundisha tabia hiyo. Nimekuiga sasa.”Vero alijibu na kuongezea kicheko kirefu huku Daktari akiondoka na kuwaacha mule wodini wakiendelea kutaniana.
******
BAADA YA MIEZI MITATU.

Hali ya Mama Vero ilikuwa imetengamaa na sasa alikuwa mbele ya umati wa watu akitoa wasaha wake kwenda kwa mwanaye mpendwa Vero, baada ya mwana huyo kufunga pingu za maisha na mtu aliyemuita muokozi wa maisha yake.

“Mwanangu Vero,endelea kupigania nafsi za wengine kama nilivyopigania mimi. Nimekulea katika malezi hayo na ndio maana leo hii umenipigania mimi. Sina cha kukulipa na wala sihitaji malipo yako,umelipa mengi sana ambayo hapo mwanzo sikufahamu kama uliwahi kufanya hivyo.”Mama Vero aliongea na kisha aliangalia sehemu fulani iliyopo mle ukimbini,na moja kwa moja alimuona Daktari aliyemtibia hadi siku ile amesimama pale.

“Namshukuru sana Daktari wangu aliyekuwa ananiangalia hadi leo hii nimesimama hapa mbele yenu. Nilikuwa wa kufa lakini Daktari hakukata tamaa licha ya miezi mitano niliyokaa kitandani bila kujitambua. Nakushukuru sana Daktari Pondamali Mwafute. MUNGU akujaze roho hiyohiyo.”Mama Vero aliongea mengi sana usiku ule lakini mengi yalikuwa ni ushauri pamoja na mahaso.

Taarifa ya Daktari kuhusu ugonjwa wa mama yule.ilisema kuwa Mama Vero alikuwa anasumu ya tetenasi ambayo haikupona kipindi kile cha nyuma,hiyo ndio ilimlaza mama yule kwa miezi mitano. Lakini aliwatoa hofu baada ya kuwaambia kuwa hali hiyo haitotokea tena kutokana na tiba alizompa mama yule.

Jina halisi la Mama Veronica ni Sarafina Sauti huku mwanaye akiitwa Veronica Tambo na watoto wake mapacha waliitwa Prince na Princess. Baba wa Prince na Princess aliitwa John Boaz,raia wa Uholanzi.

MWISHO.

Hakuna maoni:
Write maoni