RIWAYA: Daima
NA: Frank Masai
MAWASILIANO: 0717 738973
SEHEMU YA 1
Hisia za mapenzi hujengwa pale mioyo ya wawili inapokuja
pamoja na kujigundua kuwa inaendana. Hisia za mapenzi ndizo hujenga mapenzi na
kuyafanya yaishi katika mioyo ya wawili waliokutana katika dunia hii ambayo
watu huuita kila jina zuri na baya.
Mapenzi ni njia ambayo kila moyo hupenda kuipita hata bila
kutaka. Na katika kila moyo ambao unajiingiza katika mapenzi, basi kuna moyo
unapitia magumu ambayo huweza kutiririsha machozi wakati magumu hayo yanapita.
Wanasema penzi la kweli si rahisi kufa. Usemi huu ni kweli
na hamna cha kukataa katika hili. Pale mioyo miwili inapokuja na kuungana, basi
hutengeza kitu ka bomu la nyukilia, linapolipuka basi huwa maafa na uharibifu
mkubwa.
Wapo wanaodhani mapenzi ya wawili ni lazima yanedane na
dini, kabila, elimu au kipato. Na wapo wanaodhani kuwa mapenzi hayaendani na
hivi vitu. Wengi wataungana na kauli ya mwisho, labda kwa sababu hawajui sera
za familia fulani. Mimi ni mmoja wao nisiyeamini kuwa mapenzi yanajengwa kwa
njia za kuangalia dini, kabila au kipato na elimu.
Kama na wewe unaamini hili, ni vipi unaweza kupigana
kuliokoa penzi lililomea katika mioyo yenu? Kama mmoja ambaye siamini kuhusu
udini, kabila, ukipato na elimu, naweza kumshauri yule aliyetokewa na jambo
hili, apigane kufa na kupona ili kuliweka penzi lake hai.
****
Sauti ya faraja katika masikio ya mama mmoja ambaye alikuwa
hoi taabani katika hospitali moja ya nchi ya Tanzania, ilipenya katika ngoma zake
na hapo hapo alishusha pumzi ndefu ya imani na kujilaza kifudi fudi katika
kitanda cha hospitali ile.
Alikuwa amekaa katika hospitali ile kwa jumla ya siku tano
bila kufanikiwa katika kile ambacho kilimpeleka pale.
Alikuwa kafikisha siku za kuweza kujifungua na ndipo
alipokimbizwa hospitali ile kwa msaada wa wasamaria wema ambao siku zote
walilipa fadhila ambazo mama yule alikuwa anazitenda kwao. Hata wauguzi
walipomuona mama yule ndiye kaletwa kwa ajili ya kujifungua, walikuwa wenye
kila hali ya utu katika kumpa huduma mama yule ambaye licha ya kutokuwa na kitu
katika maisha yake, hasa hivi vya kuonekana lakini moyo na kichwa chake vilijaa
ubinadamu wa kutosha. Alikuwa na ulimi wa kuweza kumfanya nyoka asiweze
kumng’ata liyemdhamiria. Alikuwa na kinywa safi ambacho ndicho kilimfanya aheshimike
na kila mtu, kila rika na kila jinsia.
Sauti ya mtoto mchanga, ilisikika ikilia kwa nguvu baada ya
kutoka tumboni kwa mama yake. Wauguzi waliyobeba jukumu la kumleta mwana yule
duniani, walitabasamu na kumtazama mama aliyehusika kumlea mwana yule kwa miezi
tisa akiwa tumboni. Wakatabasamu zaidi pale mama yule alipowauliza kwa sauti ya
kichovu kuhusu jinsia ya mwana yule.
“Ni wa kiume.” Alijibu muuguzi mmoja wa kike aliyekuwa
kamkamata mtoto na mama yule alitabasamu pamoja na wauguzi, kisha kwa sababu ya
kutumia nguvu nyingi kwa kumleta duniani mwana yule, alifumba macho yake, mama
yule alipoteza fahamu..
****
Jogoo aliwika katika nyumba moja kuu-kuu iliyokuwa imeezekwa
kwa nyasi juu yake, na kujengwa kwa tope bila tofali. Jogoo kuwika ilikuwa ni
ishara ya mapambazuko, ilikuwa ni sauti ya kuwakumbusha watu waamke na kwenda
eidha kulijenga taifa au kulisafisha taifa. Ni siku mpya ilikuwa inaanza, siku
ambayo nyumba hii ilipata mgeni mpya, mgeni ambaye aliletwa na mama pendwa
katika sehemu ile anayoishi.
Aliyekabidhiwa kuitazama nyumba ile kwa wema, alidamka baada
ya jogoo kuwika mara kadhaa, na kitendo bila kuchelewa alianza kazi ya usafi wa
mazingira ya nje ya nyumba ile. Alionekana wazi alikuwa na hamasa ya jambo fulani
kwani hata wakati fagio linatambaa katika ardhi ile kuondoa uchafu, yeye
hakuwepo katika dunia hii na badala yake alikuwa anafagia huku ametabasamu kana
kwamba hukujali vumbi zito lililokuwa linapenya katika kinywa na pua zake.
Alikuwa na furaha mwanamama yule.
Ni wiki mbili zilitimia tangu mama yule wa hospitali apate
mtoto wa kiume. Alipata huduma za kutosha toka katika hospitali ile. Wauguzi
walitamani mama yule asiondoke katika hospitali ile, lakini walikuwa hawana
jinsi kwani muda uliwadia wa mama yule kuanza majukumu mapya ya kumlea mwana
wake wa pekee.
Saa nne ya asubuhi, mama aliyekuwa anafagia nje ya nyumba
iliyokuwa inaonekana inaukwasi, alifika katika hospitali aliyokuwa kalazwa mama
mwenye kiumbe mpya na kumchukua rafiki yake kipenzi tayari kwa kurudi naye
nyumbani. Wauguzi waliwapungia mikono ya kheri wakati wazazi wale wanaingia
ndani ya usafiri utakao wafikisha nyumbani kwao. Nao wakinamama wale, walijibu
kwa kuwapungia mikono pia. Safari ya kwenda kwao ikashika hatamu.
****
Ni furaha kubwa ndio ilikuwa imetawala katika nyumba ya mama
aliyekuwa kajifungua. Wakina mama wenzake walipiga vigeregere kila mara
walipopata jambo la kujenga. Waume walikuwa wanamiminika na kumpongeza mama
yule kwa kumpa chochote cha kheri. Kheri hiyo ndio ilifanya vigeregere
kutokwama katika ndimi za wakina mama wale.
“Mwana wetu anaitwa nani huyu,” Baba mmoja wa makamo
alimuuliza mama wa mtoto pale alipoenda kumtembelea.
“Anaitwa Samson.” Mama yule alimjibu mzee yule huku tabasamu
pana likichomoza katika midomo yake pevu.
“Oooh! Samson!” Mzee yule aliongea huku akisogeza uso wake
kwa yule mtoto. “Ni jina la shujaa wa MUNGU. Yule bwana jabari aliyeweza
kupambana na simba, kisha akamteketeza bila huruma. Hakutumia silaha katika
mpambano wake, ni mikono pekee,” Mzee yule aliongea zaidi huku safari hii
akikunja ngumi kuonesha ukakamavu wa kitu ambacho alikuwa anakihadithia.
Akaendelea,
“Nadhani MUNGU kamleta shujaa huyu kupambana katika maisha
haya. MUNGU kamtuma mwana huyu kwa ajili ya jambo la kishujaa. Naamini
atalitimiza. Samson karudi tena.” Maneno hayo yakaamsha vigeregere tena na mama
yule alichemka mwili kwa dezo baada ya sifa kede zilizomwagwa na mzee yule.
“Ahsante Mzee Shahibu.” Mama yule alimshukuru mzee yule kwa
maneno yake.
“Hapana. Siruhusiwi kushukuriwa, bali kukushukuru wewe
kutuletea shujaa. Asante Mama Samson.” Mzee yule aliongea huku akipiga goti na
kushika miguu ya Mama Samson.
Hoihoi zikaibuka tena na mama yule alishindwa kustahimili
hali ile, akajikuta akitoa machozi, machozi ya furaha.
Chozi ni ishara ya hisia zinazotokana na jambo fulani. Chozi
litokapo humaanisha kuguswa na jambo fulani ambalo ni hisia pekee ndizo
hutambua siri hiyo. Hakuna chozi liwezalo kudondoka bila kuhusisha hisia.
Achana na chozi litokalo labda kwa sababu ya kulala au kuumwa mafua, hapa
nazungumzia chozi la hisia ya jambo fulani.
Mama Samson alitoa chozi la hisia za furaha iliyogubikwa
katika moyo wake. Hana pesa, hana maisha bora kama wengine, hana kitu chochote
cha kumfanya naye azungumzwe mtaani kama tajiri au mtu fulani maarufu. Lakini
rafiki zake na majirani, walimuonesha upendo wa dhati licha ya hali yake.
******
BAADA YA MIAKA SABA.
Kikundi kidogo cha watoto kilionekana kikicheza mpira wa
manailoni eneo moja lililokuwa lina uwazi mpana wa uwanja. Watoto walifurahia
mchezo ule na walitamani usiishe hata kidogo kwani ni starehe moja iliyokuwa
inaviweka vichwa vyao sawa.
Wakati mchezo ukizidi kunoga baina ya watoto wale, gari moja
kubwa linajongea katika nyumba moja kubwa ambayo ilikuwa imejengwa mitaa ile. Ilikuwa
ni nyumba kubwa kupita nyumba zote zilizopo pale mtaani. Ilizunguishiwa uzio
mpana wa matofari na nyaya za umeme ziliwaka kila nukta moja ya sekunde ya saa.
Gari ile pana ilisimama nje ya geti na kwa dakika tatu
hakushuka mtu hadi pale gari lingine la kifahari lilipojongea na kusimama nyuma
ya gari lile kubwa.
Dereva wa gari kubwa alishuka na kwenda kufungua geti lakini
kwa bahati mbaya, gari lile pana na refu kwenda juu, likashindwa kuingia ndani
na jukumu kubwa lilikuwa ni kutafuta vijana ambao wangeweza kufanya kazi ya
kupakuwa na kuingiza ndani baadhi ya vifaa vidogo vidogo.
Watoto waliacha kucheza mpira na kuanza kuangalia uzuri wa
gari lililofuatana na lile la mizigo. Wakawa wanalitamani na wengine
walilipapasa kwa mshangao mkubwa.
“Watoto, mnaweza kutusaidia kupeleka vitu ndani?” Aliwauliza
dereva wa gari kubwa na watoto wote walijibu kwa haraka kuwa wanaweza.
Wakatafutwa na vijana wengine wakubwa na kuanza kushusha
mizigo iliyomo kwenye gari. Gari la kifahari liliingizwa ndani na kuwekwa
sehemu yake wakati huo watoto walipishana mara kwa mara mlangoni wakiwa wamebeba
vitu vya kuingiza ndani.
Katika gari lile la kifahari, mlango wa dereva unafunguliwa
na bwana mmoja mrefu na mweusi kiasi akatoka nje akiwa katika mavazi ya gharama
labda kushinda ya yeyote katika mtaa ule. Kiatu kirefu cha ngozi ya chatu
kinadondokea ardhi na bwana yule anatabasamu baada ya kuangaza huku na huko
kwenye ile nyumba.
Upande wa pili baada wa dereva, mlango pia unafunguliwa na
anashuka mwanadada mrembo kupindukia, naye akiwa katika mavazi ya gharama kama
aliyeshuka upande wa dereva. Huyu alikuwa na asili ya kiarabu kutokana na
nywele zake ndefu pamoja na weupe wa asili ambao MUNGU kamuumba nao.
“Abdul, umefanya vema sana mume wangu.” Mwanamke yule
aliongea huku kapambwa na tabasamu pana ambalo siku zote alikuwa akilichanua,
mumewe kipenzi, Bwana Abdul Abdulah, mmiliki wa makampuni makubwa ya biashara
nchini Tanzania, alikuwa hachomoki wala kufikiria kwenda nje ya ndoa yake.
“Tumefanya wote haya mke wangu Johari,” Naye mumewe alijibu
huku akibusu midomo mipana ya mkewe ambaye naye si haba, alikuwa anafukuzana na
mumewe katika ujasiriamali.
Wakati hayo yanaendelea, mlango wa abiria wa gari lao nao
unafunguka na mtoto wa miaka ipatayo sita anashuka ndani ya gari lile. Alikuwa
ni mtoto wa kike ambaye alichukua sura nzuri ya mwanamke anayepongezana na
Abdul, namzungumzia Johari Said Mustapha.
“Baba hapa ndio kwetu kupya?” Mtoto yule alimuuliza baba
yake, Bwana Abdul.
“Ndio Fatma. Utakaa hapa na dada zako wa kule,” Aliongea
Abdul huku akijaribu kumwambia kuwa atakaa na wafanyakazi aliotoka nao huko.
Mtoto yule akatabasamu na kuanza kuangaza huku na huko ndani
ya mjengo ule ambao kwa hakika ulijengwa kwa ustadi na ramani za kileo zaidi.
Wakati Fatma anaendelea kuzagaa pale uwani akiitazama nyumba
ile juu ya bati na anga zima la pale alipohamia, alijikuta akigongana na mtu
ambaye hakumjua hapo kabla.
Alikuwa ni mtoto
usawa wake, lakini yeye ni wa kiume na alikuwa kabeba baadhi ya vitu
vidogovidogo vya kupeleka ndani ya nyumba ile.
Akamtazama yule mvulana kwa macho yake machanga, na mvulana
yule akamtazama pia. Macho yao yakagongana. Wote kwa pamoja wakabaki hawana la
kusema.
“Sam peleka vitu ndani,” Ni sauti ya mtoto mwingine ilimsihi
mtoto mwenzake apeleke vitu ambavyo kavikamata mikononi mwake.
Alikuwa Samson, kijana anayelelewa katika mazingira magumu
akiwa na mama yake. Samson akatabasamu mbele ya Fatma, na Fatma akajibu
tabasamu lile kwa kukenua hadi mapengo yake ya mbele yakaonekana. Samson
akaingiza vitu vile ndani.
ITAENDELEA.
Hakuna maoni:
Write maoni