Jumanne, 31 Mei 2016

ACT WAZALENDO WATOA TAMKO-ZITTO KUSIMAMISHWA KUSHIRIKI VIKAO VYA BUNGE



Baada ya kutoka kwa taarifa kuwa wabunge Zitto Kabwe na Halima Mdee kuzuiliwa kuingia bungeni katika bunge la bajeti, Chama cha ACT-Wazalendo kimetoa taarifa kuhusu kusimamishwa kwa wabunge hao ambapo mojawapo ni Kiongozi Mkuu wa chama chao, Mh. Zitto Kabwe.

Katika taarifa ambayo imetolewa na Katibu wa Itikkadi, Uenezi na Mawasiliano, Ado Sgaibu kupitia ukurasa wa Facebook wa ACT amesema chama chao kimesikitishwa kwa kitendo hicho lakini kwa upande mwingine wanafarijika kwa kuona wanafanyiwa hivyo kwa kuwatetea wananchi.
“Chama cha ACT Wazalendo kimesikitishwa na kitendo cha ugandamizaji wa demokrasia kilichofanywa na wabunge wa CCM kwa kuwasimamisha ubunge wabunge wa upinzani akiwemo kiongozi wa chama chetu ndg. Zitto Kabwe,
Katikati ya masikitiko hayo tunafarijika kuona wabunge hao wameondolewa kwa sababu ya misimamo yao ya kutetea maslahi ya wananchi, tungesikitishwa zaidi kama mashujaa wetu hawa wangeondolewa bungeni kwa sababu ya ulevi au wawe sehemu ya wagonga mihuri ya masuala ya hovyo hovyo yanayosimamiwa na serikali ya chama cha Mapinduzi (CCM),” ilisema taarifa hiyo.
Pia katika taarifa hiyo ACT wameeleza kuwa wanaandaa maandamano yatakayofanyika Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapokea wabunge ambao wametolewa bungeni kwa sababu ya kuwatetea wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
“Kwa sababu hiyo ya kusimamia maslahi ya wananchi sisi kwetu ni mashujaa na kwa maana hiyo Chama chetu kinaandaa maandamano makubwa jijini Dar Es Salaam kuwapokea mashujaa wa wananchi,” ilieleza taarifa hiyo.

Hakuna maoni:
Write maoni