Jumatatu, 30 Mei 2016

MJUE MWANDISHI NA KALAMU YAKE

MJUE MWANDISHI NA KALAMU YAKE


Habari za wakati huu wapenzi wa riwaya... Naam, nakukaribisheni kwenye makala yetu hii ya 'MJUE MWANDISHI NA KALAMU YAKE' ninae kuletea makala hii ni mimi Zubery Razuur Mavugo.


MAKALA Leo katika makala yetu tutayatazamia maisha ya Mwandishi kwa jina la HASSAN OMARI MAMBOSASA.

HISTORIA YA MAISHA YAKE KIUFUPI

Jina lake kamili anaitwa Hassan Omari Mambosasa, ni mzaliwa wa nne katika familia ya mzee Omari, lakini pia ni mzaliwa wa kwanza upande wa Mama yake kipenzi Bi. Swaumu Mohamed Suleiman. Amezaliwa tarehe 14 februali mwaka 1993 katika Hospitali ya Ngamiani huko Tanga. Alianza kusoma elimu yake ya msingi mnamo mwaka 1999 katika shule ya msingi Koboko. Kutokana na kurudishwa darasa la kwanza kwa mara ya pili kulimpelekea ahitimu darasa la saba mwaka 2006 katika shule ya msingi Kizuiani iliyopo Mbagala.
Elimu ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne amepitia shule tatu tofauti, ambazo ni ; Jitegemee, Ubungo islamic na Wailesi kitendo kilichomfanya akariri kidato cha pili kutokana na kuhamishwa shule moja kwenda nyingine. Alihitimu kidato cha nne mwaka 2011.
‘’Nilianza kidato cha tano shule ya sekondari Tambaza hadi nilipohitimu mwaka 2014 kisha nikajiunga na Jeshi la kujenga Taifa kwa mafunzo mafupi.’’ Mambosasa alisema.
Mambosasa mpaka sasa ana elimu ya kidato cha sita ambayo tayari amesha ikamilisha, lakini pia bado anasoma, yupo Chuo. Anasomea ‘Computer Science’ huko Songea, ndani ya chuo kijulikanacho kwa jina la ST. Joseph.

NDOTO ZA KUWA MTUNZI WA MAANDISHI

Ndoto za kuandika zilimjia punde tu baada ya kumuona rafiki yake kipenzi [hatujafanikiwa kulitambua jina lake kwakuwa makala yetu ni mbegu] ambaye alikuwa mchoraji mwenzake; rafiki yake huyo alikuwa akipenda kuchora kisha anaandika maandishi kwenye mchoro aliyo uchora, kitendo kilichomvutia sana Hassan na hapo ndipo aliposhawishika kwa kiasi kikubwa kuandika, ingawa alikuwa akichukulia kama sehemu yake ya kujifurahisha tu. Lakini siku nenda siku rudi ndipo alipokuja kugundua kipaji chake.

HADITHI YAKE YA KWANZA.

Hassani Mambosasa ingawa alikuwa akipenda kuandika lakini hakuwa amewahi kuandika hadithi nzima japokuwa kila siku, saa na hata dakika hadithi zilikuwa zikijitunga kichwani mwake.
‘’Hadithi yangu ya kwanza ilikuwa ikiitwa JOKA LA AJABU niliiandika kwenye karatasi ambazo nilizikunja mara mbili zikawa zipo kwenye mfumo wa kitabu.’’ Mambosasa alisema siku moja baada ya kutembelewa na mmoja kati ya watoa habari wetu wa kutoka hapahapa Becker tv

KUJIINGIZA, MTANDAONI.

Hassani Mambosasa anasema kuwa, alijiingiza mtandaoni akiwa kama mtu wa kawaida tu aliyetaka kuwasiliana na watu mbalimbali pamoja na kupata marafiki wapya. Akiwa kwenye pitapita zake hapa na pale ndipo alipokutana na ukurasa ambao hapo zamani ulijulikana kwa jina la Kona ya Riwaya ingawa hivi sasa unajulikana kwa jina la Kona ya Riwaya ‘reloaded’, huko ndiko alikoshawishika na yeye kuandika riwaya mtandaoni kwa mara ya kwanza kabisa. Hadithi yake ya kwanza kuiandika mtandaoni ilijulikana kwa jina la SADAKA na hiyo ni baada ya kupata ushawishi na hamasa kutoka kwenye ukurasa wa kona ya riwaya.

CHANGAMOTO.

‘’Changamoto nilizopitia ni nyingi sana lakini muda pamoja na ukosefu wa kitendea kazi hapo kipindi cha nyuma ndivyo vilinisumbua sana’’ Hassani alisema baada ya kuhojiwa na mwandishi wetu wa makala ya mjue mwandishi na kalamu yake

MAFANIKIO.

‘’Mafanikio sina makubwa sana kiasi cha kuweza kuyatangaza lakini napenda niseme tu kupitia uandishi nimejikuta nikisogea kwenye hatua moja nzuri sana.’’ Mambosasa alisema.

ANACHOSEMA KWA MASHABIKI ZAKE.

'’Ninachowaambia mashabiki zangu ni kwamba, waendelee kuwa nami kwani kuna vizuri vinakuja zaidi ya wanavyovisoma, lakini pia naomba wazidi kunipatia sapoti yao kwani hakuna fanani bila hadhira hata siku moja.’’ Alisema.

BAADHI YA KAZI ZAKE NI;

NSUNGI.
WAKALA WA GIZA.
WITO WA KUZIMU.
SHUJAA.
SHUHUDA.
KOSA.
DHAHAMA.
JINAMIZI.
NA NYINGINEZO NYINGI......

Hakuna maoni:
Write maoni