Jumapili, 29 Mei 2016

UREMBO NA MAVAZI YA MSICHANA


Ingawa ni vigumu kueleza kinagaubaga maana halisi ya neno urembo, naweza kusema kuwa urembo ni utumiaji wa mapambo, manukato, marashi, uturi, mavazi na rangi ili kuremba na kuongeza nakshi na umaridadi katika mwonekano, sifa na viwango vya ubora wa msichana au mwanamke kwa lengo la kuvutia au kufurahisha hisia (za kuona, kunusa au kugusa) za mtu mwingine atakayekutana naye.
Urembo ni swala linalotokana na mtazamo wa jamii kwa wakati uliopo, ni kile jamii inachoamini kuwa kinavutia hisia hata kama kwa hakika si urembo katika jamii nyingine. Kwa maana hiyo vipodozi na mavazi ni vitu muhimu sana katia maswala ya urembo.
Katika siku za hivi karibuni urembo pia huchukuliwa kama biashara na fani inayozalisha ajira kwa ajili ya kuwaongezea kipato wasichana wanaotimiza vigezo na matarajio ya matajiri wanaoandaa mashindano ya urembo.
Ingawa katika mashindano ya urembo waandaaji huipamba zaidi maana ya neno urembo na kuiongezea vipengele na vigezo kama vile msichana ambaye hajaolewa au kuzaa, mwenye kipaji, elimu nzuri ya darasani na mwenye uwezo wa kujieleza, lakini maana halisi ya urembo inabaki bila kuathiriwa. Urembo wa msichana hauwezi kutenganishwa na mvuto wa mwonekano wake.

Vipodozi

Ni jambo la kawaida na linalofaa kwa sisi binadamu kuhangaikia sura na mwonekano wetu, Mungu alipotuumba aliweka ndani ya mioyo yetu shauku ya kupenda uzuri na kupendeza. Alitupatia pia vitu vya asili na salama kwa ajili ya kutufanya tuendelee kuwa wazuri; Yeye ndiye aliyeumba dhahabu, almasi, lulu, maua yanayotoa harufu nzuri na mimea yenye mafuta na manukato salama ili tuvitumie kwa faida.
Msichana anayejali afya yake ni lazima azingatie usafi na mwonekano wake. Ni lazima aitunze ngozi yake, nywele zake na kucha katika hali inayovutia, kupendeza na kudumisha afya. Msichana yeyote hapaswi kukaa katika hali ya uchafu na kujisahau kiasi kwamba watu wengine wakaudharau usichana wake.
Hapa ndipo swala la wasichana kuwa watumiaji na wateja wakuu wa vipodozi linapoingia. Ni jambo zuri kutumia vipodozi, hata vitabu vya kumbukumbu za zama zilizopita vinatutaarifu kuwa wasichana wa zamani walioheshimika walitumia vipodozi salama [8]. Paulo, mwanazuoni na mwanasheria wa karne ya kwanza pia aliwashauri wanawake kutunza nywele zao vizuri [9].
Ni jambo la busara kuelewa kuwa lengo la kutumia vipodozi si kujipamba kwa ajili ya urembo wa kupendeza tu wala si kuiga mwonekano wa mitindo na matangazo ya biashara katika majarida na matangazo ya biashara bali pia ni kwa ajili ya afya njema. Hivyo basi ni vema na haki kuvifahamu, kuchagua na kutumia vipodozi salama kwa afya ya mwili, akili na roho.
Kuangaikia sura kupita kiasi kwa kujiangalia kwenye kioo, kutengeneza au kuvaa nywele za bandia, kuvaa mavazi yenye mitindo ya aina mbalimbali ya kisasa na kujipaka vipodozi kupita kiasi ni tatizo la afya ya akili na hisia sawa na tatizo la urahibu wa dawa za kulevya.
Msichana wa leo anayejali afya yake hana haja ya kuubadili mwili wake au kufanya marekebisho ya maumbile ya ngozi na sura yake ya asili kutokana na maoni ya wanamitindo wanaofanya biashara kwa faida zao za kibinafsi katika mfumo wa maisha ya kibepari bila kujali afya za wateja wao. Hakuna sababu za msingi kwa msichana kutekwa fikra zake kitumwa na waandaaji wa mashindano ya urembo au kuviachia vyombo vya habari viamue sura na maisha yake yatakavyokuwa.
Mwandishi mmoja maarufu sana duniani na mwelimishaji wa mambo ya afya ya mwili na roho, aliwahi kusema kwamba msichana anayejinasua katika utumwa wa mitindo ya kisasa (fashions), atakuwa pambo zuri sana katika jamii yake [10]. Mitindo ya kisasa inaleta urahibu na kufanya mtu kuwa mtumwa wa wafanyabiashara wanaoandaa matangazo ya biashara kwa ufundi mkubwa ili kujipatia mawindo yao.
Ingawa ugonjwa wa kuangaikia sura kupita kiasi huwapata watu wa umri wowote, kwa kawaida vijana hasa wasichana huathiriwa zaidi na hali hii. Matumizi ya vipodozi yana uhusiano wa karibu sana na afya ya ngozi, afya ya mfumo wa fahamu na afya ya mfumo wa damu kutegemea kiasi, njia ya kutumia na urefu wa kipindi cha kutumia.
Ngozi yenye afya ina kazi nyingi ikiwa ni pamoja na kulinda mwili dhidi ya mashambulizi ya bakteria na vimelea wengine wanaosababisha magonjwa. Ngozi pia husaidia mwili usipate madhara yatokanayo na mionzi ya jua na kuzuia ugonjwa wa saratani (kansa). Kazi zingine za ngozi ni pamoja na kutoa uchafu mwilini, kusaidia katika mawasiliaono yasiyohitaji maneno, kurekebisha joto la mwili na kusafirisha hisia za mwili. Ngozi pia huzalisha mafuta yanayo lainisha mwili, huzalisha kinga mwilini na kutengeneza vitamini D ambayo ni ya muhimu sana kwa afya ya mifupa, meno na misuli.
Afya ya ngozi, nywele na kucha hutegemea sana mazingira ya ndani na nje ya mwili, hutegemea umri, jinsia, lishe, kinga mwili, vinasaba, kazi, usafi, hali ya uchumi, hali ya hewa, mila, mazingira na matumizi ya vipodozi.
Tatizo kubwa la vipodozi vingi leo kwa afya ya wasichana linakuja pale msichana atakapotumia vipodozi vyenye viambato vyenye sumu na dawa vinavyochubua ngozi na kuharibu rangi ya asili ya ngozi, kucha na nywele. Na hali hii husababisha madhara ya kiafya mapema sana au baadaye sana. Vipodozi vingi vya leo wanavyotumia wasichana vimechanganywa na sumu ya ‘hydroquinone’ pamoja na viambato vya dawa za ngozi na rangi zisizofaa kwa matumizi ya binadamu.
Vipodozi vingi huathiri ubora wa afya ya ngozi na kusababisha ngozi kuwa na mabakamabaka, ngozi kukunjamana na kupoteza hali yake ya kuvutia. Ngozi pia huwa nyembamba sana na kulainika kuliko kawaida. Hali hii husababisha ngozi kuchanika kwa urahisi na kushoneka kwa shida pale mtumiaji anapopata jeraha kubwa linalohitaji matibabu ya kushona. Ngozi iliyolainishwa sana kwa kemikali huzeeka haraka na kukunjamana baada ya miaka michache ya kutumia vipodozi vyenye kemikali hizo.
Vipodozi vingi pia huleta weupe bandia wa mwili kwa kuondosha dawa ya melanin inayofanya ngozi ya mwafrika kuwa nyeusi ambayo kimsingi humsaidia kukabiliana na mionzi ya jua. Ngozi isiyokuwa na melanin ya kutosha huathiriwa na mionzi ya jua kwa urahisi na kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa saratani (kansa) ya ngozi kwa urahisi.
Matumizi ya vipodozi hivi hatari pia yanaweza kusababisha kansa ya damu, kansa ya mapafu, kansa ya ini, kansa ya ubongo na uvimbe ndani ya pua (nasal polyps). Madhara mengine ya vipodozi visivyofaa ni pamoja na kupata chunusi kubwa, kupata ugonjwa wa mzio wa ngozi (allergy) na mwili kuwasha mara kwa mara. Vipodozi vyenye harufu kali pia vinaweza kusababisha ugonjwa wa pumu na kikohozi kwa mtumiaji au kwa watoto wadogo hasa wale wanaonyonya.
Pafyumu nyingi zina viambato vya manukato bandia yatokanayo na kemikali zinazodhuru afya ya neva, na wakati mwingine husababisha matatizo katika mfumo wa damu, na kuharibu utaratibu mzuri wa msukumo wa damu pamoja na kusababisha maumivu ya kichwa na kizunguzungu.
Vipodozi vyenye viambato vya dawa vikitumiwa kwa muda mrefu zaidi ya majuma mawili vinaweza kusababisha hali ya kukosekana kwa ulinganifu na usawaziko wa vichocheo vya ujinsia katika mwili wa msichana. Hali hii husababisha baadhi ya wasichana kuwa na misitari au milia ya ngozi katika baadhi ya sehemu za mwili pamoja na dalili au tabia za kiume kama vile kuota ndevu, kunenepa kwa kisanduku cha sauti (Adam’s apple) na kuwa na sauti nene yenye mikwaruzo au besi.
Mabadiliko mengine huusisha kunenepa kwa kinembe (clitoromegaly) na mabadiliko katika upataji wa damu ya hedhi. Msichana anaweza kupata damu ya hedhi kidogo, anaweza asiione kabisa au damu inaweza kutoka bila mpangilio maalumu, jambo hili linaweza kusababisha mahangaiko ya kihisia kwa msichana, na wasichana wengi huenda kuonana na madaktari mara kwa mara kutokana na athari hizi za vipodozi.
Mamlaka ya chakula na dawa Tanzania [TFDA], wenye dhamana ya kisheria ya kulinda afya ya watumiaji wa dawa, vipodozi na vyakula katika taifa la Tanzania, wamepiga marufuku matumizi ya cream, jeli, mafuta ya kujipaka, sabuni na lotion zenye kiambato cha Hydroquinone. Pia sabuni na cream zenye zebaki na homoni ya steroid zimepigwa marufuku kwa matumizi ya binadamu nchiniTanzania, [kwa taarifa zaidi tembelea katika tovuti ya TFDA, www.tfda.or.tz].
Viambato vingine ndani ya vipodozi vinavyodhuru afya ni pamoja na Petrolatum (mineral oil), Phthalates (DMP). 1, 4 dioxane /Polyethylene Glycol(PEG), Triethanolamine (TEA) na Parabens.Viambato hivi vinaweza kusababisha athari katika mfumo wa uzazi na kupunguza uwezo wa kutunga mimba, ugonjwa wa ini na figo na kupungua kwa uwezo wa kufikiri pamoja na ubunifu.
Athari za vipodozi hivi pia ni pamoja na kupunguza uwezo wa akili katika kujifunza mambo. Tatizo jingine ni urahibu na tamaa ya kutaka kuendelea kutumia na kupoteza uwezo wa kujidhibiti dhidi ya vipodozi hatari. Akili ya mtumiaji wa vipodozi hasa vile vinavyochubua ngozi na kuleta weupe bandia huzoea hali ya kudanganywa kuwa weupe ndio uzuri na urembo kiasi kwamba haikubaliani kwa urahisi tena na muonekano wa asili.
Kukosa au kuacha matumizi ya vipodozi hivi, husababisha msongo wa mawazo na msichana hupata hisia kuwa ngozi nyeusi siyo ya kuvutia hasa kwa wanaume au wavulana. Kwa wasichana hawa ngozi nyeusi ya asili husababisha huzuni na ngozi yenye weupe wa bandia ndiyo inayoleta furaha maishani mwao bila kujali hatari za kiafya.
Ngozi nyeusi kwao humaanisha kukosa mafanikio maishani, na hili huwafanya kuwa wabaguzi wa rangi na kuaibishwa na asili yao kama watu weusi. Huu ni mwendelezo wa dhana ya ubaguzi wa rangi uliokomaa katika mfumo wa kisayansi.
Msichana mmoja mwenye asili ya Afrika anayeishi Uingereza, aliwahi kusema kuwa anachukia kuwa mtu mweusi, anatamani kama angeweza kuondoa damu yote mwilini mwake na kuimwaga pamoja na kuchuna ngozi yake nyeusi yote ili awe mweupe. (http://www.sporah.com/2012/08/i-hate-being-ablack-girl-i-wish-i-could.html).
Huu ni ushahidi tosha kuwa wasichana wanaojichubua kwa vipodozi hatari ni waathirika kiasikolojia. Lakini hii pia inaweza kutafasiriwa kama athari ya biashara ya utumwa na utawala wa kikoloni. Katika utafiti uliofanywa jijini Dar-es-Salaam Tanzania na Dr.Kelly M.Lews wa Chuo Kikuu cha Georgia cha nchini Marekani, ulibainisha kuwa miongoni mwa sababu za kukithiri kwa tatizo hili, ni athari za ukoloni na biashara ya utumwa (The Psychology of skin Bleaching in Tanzania: From Slavery to Colonization to Contemporary Motivations, 2011).

Hakuna maoni:
Write maoni